USHIRIKIANO WA WAZAZI WAWASHA MOTO WA UFAULU NGUVUMALI

July 31, 2026

 



Na Mwandishi Wetu, Tanga


WAZAZI, walezi, walimu na viongozi wa Kata ya Nguvumali jijini Tanga wameanzisha mkakati wa pamoja wenye lengo la kutokomeza matokeo ya Daraja Sifuri katika mitihani ya taifa, wakiamini ushirikiano wa wadau wote wa elimu ndiyo ufunguo wa kuongeza ufaulu wa wanafunzi.


Azimio hilo lilifikiwa katika kikao cha wazazi na walezi kilichofanyika katika Shule ya Sekondari Nguvumali, ambapo wadau hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya shule, familia na serikali za mitaa ili kuboresha matokeo ya wanafunzi wa Kidato cha Pili na Kidato cha Nne.

Akizungumza katika mkutano huo ambao uliitishwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo Ibrahim Okash, Diwani wa Kata ya Nguvumali, Mustapha Selebosi, alisema hatua hiyo inalenga kubadili taswira ya elimu katika kata hiyo kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza na kufanya vizuri katika mitihani ya taifa.


Alisema mafanikio ya wanafunzi hayawezi kupatikana bila ushiriki wa karibu wa wazazi, walezi, walimu na viongozi wa jamii.


"Siwezi kuitwa Meya wakati kata yangu inafanya vibaya katika mitihani ya taifa. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunafuatilia maendeleo ya watoto wetu na kuweka mazingira yatakayowawezesha kufanya vizuri," alisema Selebosi.

Aliongeza kuwa kuboresha mfumo wa ufundishaji, kuongeza usimamizi wa wanafunzi na kuwajibisha kila mdau wa elimu ni miongoni mwa mikakati itakayosaidia kuinua kiwango cha ufaulu katika shule za kata hiyo.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Centre for Education (TCE), Yusuf Ogutu, alisema Kata ya Nguvumali ni miongoni mwa shule 10 zilizobainika kuwa na changamoto ya ufaulu, hali iliyosababisha kujumuishwa katika mpango maalumu wa mafunzo unaolenga kuongeza uwezo wa wanafunzi kujifunza kwa ufanisi na kujiandaa vizuri kwa mitihani.


Alisema mpango huo unatekelezwa na TCE kwa kushirikiana na Botnar Foundation na Inovex kupitia mradi wa Tanga Yetu, ukiwa na lengo la kuboresha ubora wa elimu katika shule za serikali.


Kwa mujibu wa Ogutu, changamoto kubwa kwa wanafunzi wengi si ukosefu wa ufundishaji, bali ni kutofahamu namna ya kujibu maswali ya umahiri, kuelewa uzito wa mada mbalimbali na kutumia mbinu sahihi za kufanya mitihani.


"Tumekuja na mafunzo haya ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa kuelewa badala ya kukariri. Tunawafundisha namna ya kuchambua muhtasari wa masomo, kutambua mada zenye uzito katika mitihani na kuelewa matumizi ya vitenzi vinavyotumika katika maswali," alisema.


Alieleza kuwa mafunzo hayo pia yanawajengea wanafunzi uwezo wa kupanga muda wa kujisomea, kujiandaa kabla ya mtihani, kufanya mitihani kwa ufanisi na kutathmini utendaji wao baada ya kumaliza mitihani.


Ogutu alisema taasisi hiyo pia imeanza kufanya utafiti katika shule zote 27 za sekondari za serikali zilizopo Jiji la Tanga ili kubaini sababu zinazosababisha kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya Kidato cha Pili na Kidato cha Nne.


Alisema matokeo ya utafiti huo yatawezesha wadau wa elimu kuweka mikakati ya muda mrefu ya kuboresha ubora wa elimu na kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule hizo.


Naye Inspekta wa Polisi wa Kata ya Nguvumali, Sharifu Kiswamba, alisema pamoja na juhudi zinazoendelea kufanywa, utoro na tabia ya baadhi ya wanafunzi kuzurura mitaani wakati wa masomo bado ni changamoto kubwa inayochangia matokeo duni.


Aliwataka wazazi kuongeza usimamizi wa watoto wao na kushirikiana kwa karibu na walimu pamoja na viongozi wa kata ili kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo kikamilifu na kutumia muda wao kujifunza.


Hata hivyo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nguvumali Ibrahim Okash alipongeza juhudi hizo akieleza kwamba vitasaidia kuwezesha kuongezeka kwa ufaulu kutokana na ushirikiano katika jambo lolote lile ni muhimu kwa ajili ya ustawi wake.


Alisema kwamba mkutano huo ni muhimu kwa sababu unawawezesha kukutana na wazazi na walezi ili kuweza kuweka nguvu za pamoja kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ipasavyo ili kuweza kuchangia ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na pili 


Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »