Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametembelea Banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) akiwa ameambatana na Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mhe. John Malechela, Nzuguni – Dodoma.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi wa TADB, Bw. Mkani Waziri, ameelezea kuhusu mchango wa Benki katika kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia utoaji wa mikopo na huduma za kifedha zinazowawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wa minyororo ya thamani kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao.
Alieleza kuwa uwekezaji huo unalenga kuimarisha uchumi wa nchi na kuhakikisha upatikanaji wa chakula wa kutosha na endelevu.
Aidha, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Kula cha Trolle Meesle na mnufaika wa mikopo ya TADB, Bw. Daniel Amulike, ameeleza mafanikio yaliyopatikana baada ya kufadhiliwa na Benki.
Amebainisha kuwa kabla ya uwekezaji huo walikuwa wakizalisha takribani tani 30 za mafuta ya kula kwa mwezi kwa kutumia mbinu za kawaida, lakini kwa sasa, baada ya kujenga kiwanda cha kisasa kwa uwezeshaji wa TADB, uzalishaji umeongezeka hadi kufikia tani 624 za mafuta safi ya kula kwa mwezi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kuendeleza sekta ya mafuta ya kula nchini kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kuzalisha mafuta na kuimarisha uwekezaji katika uchakataji.
Alieleza kuwa hatua hizo zinalenga kuongeza uwezo wa nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula na kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje.












EmoticonEmoticon