TADB YAIMARISHA NGUVU YA WAKULIMA KUELEKEA DIRA YA MAENDELEO 2050

July 30, 2026
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema imeendelea kuimarisha nafasi yake katika kufadhili sekta ya kilimo nchini baada ya mtaji wake kuongezeka kutoka Sh bilioni 60 hadi Sh bilioni 452.16, hatua iliyowezesha kupanua utoaji wa mikopo na huduma za kifedha kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.

Akizungumza leo Julai 30, 2026 jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa mwaka 2026/2027, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na ushirikiano wa washirika wa maendeleo.

Amesema kabla ya mwaka 2021 mtaji wa benki ulikuwa Sh bilioni 60 pekee, lakini Serikali imeendelea kuuongeza kwa awamu mbalimbali ambapo mwaka 2021 iliongeza Sh bilioni 208 na kufikisha mtaji kuwa Sh bilioni 268.

Nyabundege amesema mwaka 2024 Serikali, kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), iliongeza Sh bilioni 174.16 na kufikisha mtaji kuwa Sh bilioni 442.16, huku mwaka 2025 ikiongeza tena Sh bilioni 10 na kufanya mtaji wa sasa kufikia Sh bilioni 452.16.

Mbali na mtaji wa Serikali, amesema TADB imefanikiwa kuvutia rasilimali nyingine za kifedha kupitia mikopo ya washirika wa maendeleo, ikiwemo Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), yenye thamani ya Sh bilioni 445.6.

Aidha, amesema benki inasimamia Mfuko wa Dhamana (SCGS) wenye thamani ya Sh bilioni 108.4 unaofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na AFD, pamoja na fedha za Serikali zinazosimamiwa kwa niaba yake zenye thamani ya Sh bilioni 36.54.

Nyabundege amesema ongezeko hilo la rasilimali limeiwezesha TADB kuongeza utoaji wa mikopo, ambapo asilimia 73.6 ya mikopo yote ya benki imetolewa katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025.

Amesema TADB ilianzishwa kwa lengo la kuwezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata huduma za kifedha zitakazochochea mageuzi ya sekta ya kilimo, kuongeza usalama wa chakula na kupunguza umaskini kupitia ujenzi wa minyororo ya thamani yenye tija na ushindani.

Kwa mujibu wa Nyabundege, benki itaendelea kutekeleza mikakati inayolenga kuongeza upatikanaji wa mitaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi sambamba na kukuza matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, TADB itaendelea kuwezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika biashara za kilimo, kuwekeza katika miradi inayostahimili mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ushirikiano na Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo.

Nyabundege amesema benki itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha sekta za mazao, mifugo na uvuvi zinakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Aidha, amesema TADB itaendelea kudhamini Maonesho ya Nanenane mwaka 2026 kama Mdhamini Mkuu na imewahimiza wananchi kutembelea banda la benki hiyo kwenye Maonesho Dodoma na Zanzibar ili kujionea huduma mbalimbali za kifedha na fursa zinazotolewa kwa wadau wa sekta ya kilimo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »