TEA NA UNICEF WATEKELEZA MRADI WA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 1 WA UJENZI WA VITUO 10 VYA ELIMU YA AWALI YA UFUNDI

July 22, 2026
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kushirikiana na UNICEF, inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa vituo 10 vya Elimu ya Awali ya Ufundi (IPOSA) wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja, kwa lengo la kuwapatia fursa ya mafunzo ya ufundi vijana waliokosa kunufaika na elimu ya msingi kutokana na sababu mbalimbali.

Mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Tabora, Dar es Salaam, Kigoma na Songwe. Kwa sasa, ujenzi unaendelea vizuri na umefikia hatua ya maboma katika maeneo yote ya utekelezaji.

Katika kufuatilia maendeleo ya mradi huo, kuanzia Julai 20 hadi 21, 2026, timu ya wataalamu kutoka UNICEF ikiongozwa na Mhandisi Mohamed Hindi pamoja na Afisa Elimu Bi. Jennifer Mberesero, ilifanya ziara ya ukaguzi katika miradi inayotekelezwa mkoani Dodoma. Baada ya ukaguzi huo, timu hiyo ilifanya kikao kazi na wataalamu wa TEA wanaosimamia utekelezaji wa mradi.

Lengo la kikao hicho lilikuwa kujadili hatua zilizofikiwa, kutathmini maendeleo ya utekelezaji na kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotarajiwa.

Aidha, ujumbe huo ulikutana na Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Kipesha na kumpa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mkurugenzi Mkuu Dkt. Kipesha aliwashukuru wataalamu wa TEA na UNICEF kwa usimamizi mzuri wa mradi na kuwataka kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa ndani ya muda uliopangwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »