Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Geita anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima (Nane Nane) ya Kanda ya Ziwa Magharibi yatakayofanyika Agosti 2, 2026, katika Viwanja vya Nyamhongolo vilivyopo Manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema maonesho hayo, yanayoandaliwa kwa ushirikiano kati ya mikoa ya Mwanza na Geita, yataanza Agosti 1 na kuhitimishwa Agosti 8, 2026.
Mtanda amesema maonesho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo, "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa 2050," ambayo inalenga kuwahamasisha wakulima, wafugaji na wavuvi kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko.
Amesema uzalishaji wenye tija unapaswa kuambatana na uelewa wa mahitaji ya soko, ikiwemo ubora wa bidhaa, bei na muda wa mahitaji, ili kuwawezesha wazalishaji kupanga shughuli zao kwa ufanisi na kuongeza kipato.
"Kilimo, ufugaji na uvuvi vinapaswa kuendelea kubadilika kutoka shughuli za kujikimu na kuwa biashara zenye tija zitakazochochea maendeleo ya wananchi na uchumi wa Taifa," amesema Mtanda.
Ameeleza kuwa maonesho hayo yatashirikisha mamlaka 14 za serikali za mitaa kutoka mikoa ya Mwanza na Geita, taasisi nane za fedha, taasisi 30 za serikali, kampuni 15 za zana za kilimo pamoja na kampuni za utalii na bustani za wanyama, zikiwemo Kasa Zoo na Chato Group.
Aidha, amesema zaidi ya wakulima, wafugaji na wavuvi 614 wanatarajiwa kushiriki kwa kuonesha bidhaa, huduma na teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza tija katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mtanda amewakaribisha wadau wote, wakiwemo waoneshaji, taasisi za utafiti na mafunzo, taasisi za fedha, wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi kwa ujumla, kushiriki katika maonesho hayo ili kujifunza teknolojia mpya, kubadilishana uzoefu na kutumia fursa mbalimbali za biashara zitakazopatikana.



EmoticonEmoticon