Na Oscar Assenga, Tanga
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Salum Nyamwese, amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha kila fedha inayotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo inasimamiwa kwa uadilifu na kutumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
Nyamwese ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni amesema matumizi mabaya ya fedha za umma, rushwa na ubadhirifu vinaweza kuwa kikwazo kikubwa katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Alitoa kauli hiyo mjini Tanga wakati akifungua warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoa wa Tanga iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), iliyowakutanisha wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa taasisi za umma na viongozi mbalimbali kwa ajili ya kujadili namna ya kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma.
Nyamwese alisema fedha zinazotolewa na Serikali ni mali ya wananchi, hivyo viongozi wenye dhamana wanapaswa kuhakikisha kila shilingi inatumika kwa ufanisi na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
“Fedha zinazotolewa na Serikali ni mali ya wananchi hivyo ni wajibu wa kila mkurugenzi kuhakikisha hakuna hata shilingi moja inayopotea au kutumika nje ya malengo yaliyokusudiwa. Tunapaswa kusimamia miradi kwa uadilifu na kuhakikisha wananchi wanaona thamani ya fedha zinazotolewa,” alisema.
Alisema warsha hiyo imefanyika wakati muafaka ambapo Serikali imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani, taasisi imara, uwajibikaji na matumizi yenye tija ya rasilimali za umma.
Kwa mujibu wa Nyamwese, utekelezaji wa dira hiyo hauwezi kufanikiwa iwapo viongozi hawataweka mbele maslahi ya wananchi na kupambana kikamilifu na vitendo vya rushwa, ubadhirifu na ukiukwaji wa taratibu.
“Rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo kwani huhujumu matumizi sahihi ya rasilimali za umma, hudhoofisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hupunguza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi na kuondoa imani ya wananchi kwa taasisi za Serikali,” alisema.
Aliwataka wakurugenzi kushirikiana kwa karibu na Takukuru katika kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani, kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za umma na kuchukua hatua mapema dhidi ya viashiria vya ubadhirifu.
Nyamwese alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuelekeza uwekezaji mkubwa katika Mkoa wa Tanga kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2025/2026, Mkoa wa Tanga umepokea zaidi ya Sh trilioni 3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za elimu, afya, maji, kilimo, mifugo, uvuvi, biashara, uwekezaji, miundombinu ya barabara, nishati, ardhi na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Hata hivyo, alisema kiasi hicho kikubwa cha fedha hakitakuwa na maana bila kuwepo kwa usimamizi mzuri, ufuatiliaji wa karibu na uwajibikaji wa viongozi wanaosimamia miradi hiyo.
“Fedha pekee hazileti maendeleo. Kinacholeta maendeleo ni usimamizi mzuri, ufuatiliaji wa karibu na uwajibikaji wa viongozi wanaosimamia utekelezaji wa miradi,” alisisitiza.
Aliwataka wakurugenzi kufanya tathmini za mara kwa mara za miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, kuhakikisha kazi zinafanyika kwa viwango vinavyotakiwa na kuchukua hatua dhidi ya watumishi au wakandarasi watakaobainika kukiuka sheria.
Akizungumzia fursa za maendeleo zilizopo mkoani Tanga, Nyamwese alisema mkoa huo unatarajiwa kuwa kitovu kikubwa cha biashara na uwekezaji kutokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo uboreshaji wa Bandari ya Tanga, reli ya kisasa (SGR) pamoja na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Alisema miradi hiyo itaongeza shughuli za kiuchumi na kuvutia wawekezaji wengi zaidi, hivyo viongozi wa halmashauri wanapaswa kuhakikisha mazingira ya uwazi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali yanaendelea kuimarishwa.
Awali, akizungumza katika warsha hiyo, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Ramadhan Ndwatah alisema taasisi hiyo imefanya tathmini ya miradi inayotekelezwa ndani ya Mkoa wa Tanga na kubaini baadhi ya changamoto zinazotokana na usimamizi usioridhisha.
Alisema changamoto hizo ni pamoja na ucheleweshwaji wa miradi, matumizi yasiyo sahihi ya fedha, ongezeko la gharama zisizo za lazima na kupungua kwa manufaa yaliyotarajiwa kwa wananchi.
“Licha ya mafanikio yaliyopatikana kwenye miradi ya maendeleo, bado kuna changamoto ya udhaifu katika utekelezaji wa miradi, ucheleweshwaji wa miradi kwabaadhi ya wadau wenye dhamana, kuongeza gharama zisizo za lazima na kupunguza manufaa yanayotarajiwa kwa wananchi,” alisema.
Alisema kutokana na changamoto hizo, wameona ni muhimu kukutana na wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ili kuwakumbusha wajibu wao katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi.
Aliwataka wadau wote wenye dhamana ya kusimamia miradi kushirikiana na TAKUKURU ili kutimiza azma ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali.
Mkurugenzi Tanga Jiji atoa ushauri kuhusu BOQ
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, aliiomba Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuzingatia thamani halisi ya vifaa vinavyotumika wakati wa kuandaa BOQ za miradi mbalimbali ya ujenzi, ikiwemo madarasa.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha gharama zinazowekwa kwenye miradi zinaendana na hali halisi ya soko na kusaidia utekelezaji wa miradi yenye ubora na thamani kwa wananchi.









EmoticonEmoticon