Na Oscar Assenga, Tanga
Mkoa wa Tanga unatarajia kuupokea Mwenge wa Uhuru Juni 17, mwaka huu, ambapo utakimbizwa katika halmashauri zote 11 za mkoa huo na kukagua, kuzindua pamoja na kuweka mawe ya msingi katika miradi 73 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 27.7.
Hayo yalisemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026.
Dk. Burian alisema Mwenge wa Uhuru utapokelewa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mpya, Kijiji cha Mtoro, Kata ya Tunguli wilayani Kilindi ukitokea Mkoa wa Morogoro, kabla ya kukimbizwa kwa umbali wa kilometa 1,340 katika halmashauri zote za mkoa huo.
Alisema Juni 28, mwaka huu, Mwenge huo utakabidhiwa Mkoa wa Kilimanjaro katika Uwanja wa Shule ya Msingi Hedaru.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, kati ya miradi 73 itakayofanyiwa kazi na Mwenge wa Uhuru, miradi 34 itawekewa mawe ya msingi, 26 itafunguliwa na kuzinduliwa, huku miradi 11 ya vijana na miradi miwili ya sekta ya maji ikikaguliwa.

Alifafanua kuwa miradi hiyo ina thamani ya Sh bilioni 27.76, ambapo Sh milioni 300.6 ni nguvu za wananchi, Sh bilioni 1.27 ni michango ya halmashauri, Sh bilioni 10.7 ni fedha za Serikali Kuu na Sh bilioni 15.47 ni kutoka kwa wahisani.
Akizungumzia kaulimbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu inayosema, “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo,” Dk. Burian alisema mkoa umejipanga kuhakikisha wananchi wa makundi mbalimbali wanashiriki kikamilifu katika shughuli zote za Mwenge.

“Tumewaandaa viongozi wa serikali, watumishi wa umma, viongozi wa dini, wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalumu pamoja na makundi mengine kushiriki kikamilifu kuanzia mapokezi hadi makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru,” alisema.
Aliongeza kuwa wananchi watapata fursa ya kuushika na kuukimbiza Mwenge huo kama sehemu ya kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa unaosisitizwa katika kaulimbiu ya mwaka huu.
Mbali na kuhamasisha maendeleo, alisema Mwenge wa Uhuru utaendelea kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, malaria, VVU/UKIMWI, matumizi ya dawa za kulevya na umuhimu wa lishe bora.
Dk. Burian aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kwa wingi katika maeneo ya mapokezi, miradi na mikesha mbalimbali ili kushiriki shughuli za Mwenge wa Uhuru.
“Mkoa umejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wanapata burudani na hamasa kupitia ushiriki wa wasanii na vikundi mbalimbali vya sanaa katika maeneo yote ambayo Mwenge wa Uhuru utakesha,” alisema.
Alisema kwa ujumla maandalizi ya kuupokea Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2026 yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha na mkoa uko tayari kwa shughuli zote za mbio hizo.
EmoticonEmoticon