PAULINA GEKUL AMBURUZA MTOTO KORTINI, MAHAKAMA YASIMAMISHA KESI

May 26, 2026



Na Mwandishi Wetu


BABATI — Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Babati mkoani Manyara imesitisha kusikiliza kesi ya jinai namba 291 ya mwaka 2026 iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Babati Mjini, Paulina Gekul, inayomkabili Brayton Lucas (17), baada ya kujiridhisha kuwa mshtakiwa huyo ni mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 na hivyo shauri hilo linapaswa kusikilizwa katika Mahakama ya Watoto kwa mujibu wa sheria.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Thadei Lister, kuiomba mahakama kujiridhisha kuhusu umri wa mshtakiwa kwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwemo cheti cha kuzaliwa kilichoonesha kuwa Brayton alizaliwa Novemba 12, 2008 na kwa sasa ana umri wa miaka 17 na miezi sita, tofauti na taarifa zilizokuwa katika hati ya mashtaka zilizomtaja kuwa na miaka 19.




Katika shauri hilo, Paulina Gekul alidai kuwa Brayton Lucas, ambaye alikuwa akichunga mifugo yake, alihusika katika wizi wa mbuzi 15 wenye thamani ya shilingi milioni tatu, kosa linalodaiwa kufanyika chini ya kifungu cha 268 cha sheria ya wizi wa mifugo. Kesi hiyo ilikuwa na jumla ya watuhumiwa watatu.

Mahakama pia ilielezwa kuwa mtoto huyo alikuwa amechanganywa katika shauri moja na watuhumiwa watu wazima, jambo ambalo upande wa utetezi ulidai ni kinyume na sheria zinazolinda haki za mtoto.




Baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Babati, Ahmed Mgodo, alisema mahakama imejiridhisha kuwa Brayton Lucas ni mtoto na hivyo haina mamlaka ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo. Kutokana na uamuzi huo, mahakama ilisimamisha shauri hilo dhidi ya mshtakiwa huyo na kuagiza polisi kuandaa hati mpya ya mashtaka kwa mujibu wa sheria zinazohusu watoto.

Brayton Lucas alipatiwa dhamana huku washtakiwa wawili wengine wakiendelea kushikiliwa. Wakili Thadei Lister amesema wako tayari kuendelea kumtetea mtoto huyo iwapo atafikishwa katika Mahakama ya Watoto.

Akizungumza nje ya mahakama, Wakili Thadei alisema Brayton ni mwanafunzi wa kidato cha nne ambaye alitoweka akiwa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha na wazazi wake walikuwa wakimtafuta kwa kipindi cha miezi mitatu kabla ya kupata taarifa kuwa amekamatwa Babati kwa tuhuma za wizi.

Mama mzazi wa Brayton alisema mtoto wake alitakiwa kuwa shuleni baada ya kumaliza kidato cha nne na tayari alikuwa amepangiwa shule, lakini aliondoka nyumbani bila kutoa taarifa na baada ya juhudi za muda mrefu za kumtafuta walipata taarifa kuwa alikuwa Babati akifanya kazi.


Wakati huo huo, Diwani wa Kata ya Maruvango Wilaya ya Arumeru Mashariki, Digna Nassari, amesema taarifa za kupotea kwa mtoto huyo zilikuwa zimetolewa polisi miezi mitatu kabla ya kufunguliwa kesi dhidi yake na Paulina Gekul.

Aidha, Digna amesema Brayton ni miongoni mwa watoto 16 kutoka kata hiyo waliotoroka shule, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana kuhakikisha watoto wanarudi katika mfumo wa elimu na kupata ulinzi unaostahili

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »