MKAKATI WA BARRICK WA KUWEKEZA KUPATA WATAALAMU WA TASNIA YA MADINI WAUNGWA MKONO NA WANAZUONI NA WADAU KATIKA SEKTA

August 02, 2026
Washiriki wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa mdahalo huo
Wadau mbalimbali katika sekta ya madini nchini walioshiriki katika mkutano wa wa jukwaa la tano la utekelezaji na ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini uliomalizika jijini Mwanza wametoka na maazimio mbalimbali mojawapo likiwa ni kuwekeza kupata rasilimali watu wenye ujuzi wa kisasa kwendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na ukuaji wa sekta kama ambavyo kampuni ya Barrick nchini yenye ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga tayari imeanza kutekeleza.

Kwa kutambua kuwa tasnia ya madini inajumuisha mambo mengi zaidi ya uchimbaji, Barrick kuanzia mwaka jana imeanza kufanya kazi na taasisi za juu za elimu na za kati kwa ajili ya kusuka kizazi kijacho cha wataalamu wa tasnia ya madini wazawa ambapo imefadhili wanafunzi watano wa kitanzania kusomea taaluma ya madini nje ya nchi, imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo itatoa shilingi bilioni 26 za kuleta tija na ufanisi katika kukuza tasnia kwa kuongeza tafiti,nguvu kazi ya wataalamu,ubunifu na kwa ajili ya kuwajengea wanafunzi wanaosomea fani ya madini kuanzia ngazi ya shahada ya kwanza,shahada ya uzamili na uzamivu.

Barrick pia inayo program ya wataalamu wabobezi kutoka kwenye kampuni kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosomea tasnia ya madini kwenye vyuo vikuu ambapo mapema mwaka huu yaliwafikia wanafunzi wa mwaka wa mwisho katika shule ya Madini na Jiolojia (SoMG) ya shule Kikuu cha Dar es salaam pia imekuwa inatoa nafasi kwa wanafunzi  wa vyuo vikuu na vya kati wanaosomea fani mbalimbali kufanya mafunzo ya vitendo katika migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu.

Akitoa mada ya Uzalishaji wa Rasilimali watu unaoendana na Ukuaji wa Teknolojia mpya katika sekta ya madini nchini , Mkuu wa  Shule ya Madini na Sayansi ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SOMG) Profesa Elisante Mshiu, alisema kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kwenye sekta ya madini nchini na mabadiliko ya teknolojia, wadau wote waliopo katika tasnia wanapaswa kuungana pamoja na kutambua kuwa biashara ya madini si kuchimba pekee bali kunahitajika kuwekeza kupata rasilimali watu ya kizazi kipya yenye ujuzi wa kisasa ambayo itaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia za kisasa yanayoendelea kwenye tasnia ikiwemo matumizi ya akili unde (AI).

Alisema wakati kasi ya wawekezaji katika tasnia inakuwa na kunakuwepo na sheria za kuweza wazawa kunufaika na mnyororo wa sekta suala la kuwekeza kwenye elimu haliepukiki kwa ajili ya kupata nguvu kazi yenye utaalamu kuanzia kwenye masuala ya Jiolojia, uhandisi wa madini, uchenjuaji, biashara na sheria, mifumo ya Tehama, Ugavi, usafirishaji na taaluma nyinginezo ambazo zinahusu mnyororo mzima wa kufanya kazi na biashara kwenye migodi.

Profesa Mshiu alitoa ushauri kwa makampuni yote yanayohusiana na madini na wadau wote kulipa kipaumbele suala la kushirikiana na taasisi za elimu ya juu kujenga kizazi cha wataalamu katika tasnia na kuwa tayari kutoa nafasi za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi ili wakihitimu masomo yao wawe na ujuzi wa kutosha unaohitajika katika soko kwendana na shughuli mbalimbali katika mnyoyoro mzima wa tasnia ya madini kama ambayo kampuni ya Barrick imeanza kuonyesha njia.

Naye Kamishna Msaidizi wa Tume ya Madini kutoka nchini Ghana, Victoria Awuni ambaye alikuwa mmoja wa watoa mada kutoka nje ya nchi katika mkutano huo, alisema ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini hakumaanishi kuuza huduma na bidhaa migodini tu bali kunahitajika uwekezaji wa dhati wa wadau katika kupata wataalamu wazawa wenye ujuzi wa kuendesha migodi na shughuli nyinginezo zinazohusiana na tasnia na njia ya kuwapata ni kushirikiana kwa karibu na vyuo vya elimu  sambamba na kutoa nafasi za kutosha kwa wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo kwenye migodi na makampuni yanayohusika na shughuli za migodini.

Awuni alisema Serikali ya Ghana kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya madini imekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika elimu ili kupata wataalamu wa kutosha ambapo nchi hiyo imefanikiwa kwa kuwa na wataalamu wengi ambao wanafanya kazi katika migodi mbalimbali nje  ya nchi.

Kwa upande wake,Mhadhiri kutoka shule ya madini ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Morris Hijji akiongea katika mdahalo wa ukuzaji sekta ya madini nchini, alitoa wito kwa wadau kufanya kazi kwa karibu na taasisi za elimu ya juu ili ziweze kuandaa wataalamu wanaokidhi viwango vinavyotakiwa katika soko sambamba na kutoa nafasi za kutosha kwa wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo zaidi ya nadharia tu.

“Chuo Kikuu cha UDOM tumejipanga kufanyakazi kwa karibu na wadau katika tasnia ambao watakuwa tayari kutoa ufadhili wa wanafunzi,tafiti na kutoa nafasi za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi lengo kubwa likiwa ni kufanikisha kupata wataalamu wenye ujuzi unaohitajika kwendana na mabadiliko ya teknolojia ya uendeshaji mzima wa mnyororo wa sekta ya madini nchini na sheria ya ushirikishwaji watanzania katika tasnia ya madini”,alisema Dk .Hijji.

Naye Mkuu wa Masuala ya Ugavi (Head Enterprise&Supplier) kutoka Benki ya Absa nchini Afrika kusini akitoa mada kuhusiana na huduma za ugavi wa kitaalamu na kisasa, alisema katika zama tulizonazo kunahitajika wataalamu wenye utaalamu wa kutosha katika kufanya kazi na makampuni makubwa ikiwemo migodi wanaoelewa mifumo mbalimbali ya biashara, sheria, teknolojia na jinsi ya kufanya kazi na wadau wa nje inapobidi.

Alitoa ushauri kwa wadau wote waliopo kwenye tasnia ya madini kuwekeza kwenye elimu kwa lengo la kupata wataalamu wa fani mbalimbali ili taifa liwe na wataalamu wa kutosha ikiwemo wataalamu wanaoelewa program zinazotumika katika shughuli za utafiti,uchimbaji na shughuli nyinginezo zinazohusiana na madini.

Katika hotuba ya uzinduzi wa jukwaa hilo, Waziri wa Madini Mh.Antony Mavunde alisema kuna ongezeko la uwekezaji katika sekta ya madini na matarajio ya kuanzishwa kwa migodi mipya linatarajiwa kufungua fursa zaidi kwa watanzania kupata ajira na kutoa wito kwa watoa huduma kujiandaa kwa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani, kuongeza ubora wa bidhaa, huduma na kujenga uwezo wa kushindana katika soko, huku akigusia kuwa migodi mingine mipya 13 inakwenda kufunguliwa nchini.

Waziri Mavunde  alisema serikali imeendelea  kushuhudia ongezeko la ushiriki wa Watanzania katika utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa kwenye migodi tangu kufanyika kwa maboresho ya sheria ya Madini, sera na kanuni zake za 2009 ambao unakwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Pamoja na mambo mengine aliwataka watoa huduma katika migodi hapa nchini kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa pamoja ili kuchangamkia fursa zinazoongezeka katika sekta hiyo hususani katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma bora zinazokidhi viwango vinavyohitajika na wawekezaji kwenye sekta ya madini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »