TBS YASISITIZA USALAMA WA CHAKULA KATIKA BIASHARA ZA UOKAJI (BAKERY)

May 26, 2026
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa mafunzo maalumu kwa wafanyabiashara wa bidhaa za uokaji (bakary) Mkoa wa  Dar es Salaam ili kuongeza uelewa kuhusu masuala ya viwango, kuboresha usalama wa chakula na kuimarisha ushindani wa biashara zao sambamba na kulinda afya za watumiaji.

Akifungua mafunzo hayo leo Mei 26, 2026 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, amesema hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo wafanyabiashara wa bekari kuhusu uzingatiaji wa ubora na usalama wa chakula, sambamba na kuongeza maarifa ya ujasiriamali kwa maendeleo ya sekta hiyo.

Amesema mafunzo hayo yanakwenda sambamba na jitihada za Serikali zinazolenga kuimarisha hali za maisha ya wananchi kupitia uwezeshaji wa wanawake na vijana kiuchumi, huku biashara za bekari zikitajwa kuwa miongoni mwa sekta zinazotoa ajira kwa makundi hayo.

Dkt. Katunzi amesema TBS imeendelea kutekeleza mikakati ya kuwawezesha wafanyabiashara na wazalishaji kwa kutoa elimu kuhusu viwango, usalama wa mtumiaji, utunzaji wa mazingira na uboreshaji wa biashara ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa salama na zenye kukidhi matakwa ya sheria za viwango.

Ameeleza kuwa biashara ya bidhaa za bekari imeendelea kukua kwa kasi jijini Dar es Salaam kutokana na mfumo wa maisha wa jiji hilo ambapo watu wengi hutegemea bidhaa hizo kama vitafunwa na hata sehemu ya milo yao ya kila siku. 

Hata hivyo, ameonya kuwa bidhaa hizo zinapotengenezwa bila kuzingatia usalama wa chakula zinaweza kuwa hatari kwa afya ya jamii, hususan watoto ambao ni kundi nyeti kwa magonjwa yatokanayo na uchafuzi wa chakula.

“Mazingatio ya ubora na usalama katika uzalishaji wa bidhaa za bekari yatawezesha kupunguza magonjwa yatokanayo na chakula kisicho salama na kuongeza imani ya watumiaji kwa bidhaa zinazotengenezwa,” amesema.

Aidha, Dkt. Katunzi amesema mwezi Machi 2026 TBS kupitia Kanda Maalum ya Dar es Salaam ilifanya ukaguzi katika takriban bekari 200 ili kufuatilia utekelezaji wa sheria na viwango, ambapo baadhi ya mapungufu yalibainika na kuibua hitaji la kutoa mafunzo kwa wadau hao ili kuongeza kiwango cha ukidhi wa sheria kwa hiari na kuimarisha mazingira ya biashara.

Amesisitiza kuwa uzingatiaji wa viwango si suala la afya pekee bali ni msingi muhimu wa mafanikio ya biashara kwani huongeza ubora wa bidhaa, kuridhisha wateja na kuwezesha ushindani sawa katika soko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Katunzi amewahimiza wafanyabiashara wa sekta hiyo kuhamia matumizi ya nishati safi, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji, kuhifadhi mazingira na kulinda afya za watumiaji pamoja na wanaofanya kazi katika mazingira ya uzalishaji.

Pamoja na hayo amewakumbusha wadau hao kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya usalama wa chakula duniani yanayofanyika kila mwaka Juni 7, akisisitiza wajibu wa kila mdau kuhakikisha usalama wa chakula katika mnyororo mzima wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »