KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema kuwa uwekezaji unaofanywa na Oryx Energies Tanzania Limited ni kielelezo cha mafanikio ya juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta binafsi na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Hayo yameelezwa leo Mei 9,2026 jijini Dar es Salaam wakati Kamati hiyo ilipotembelea sehemu maalumu ya uzalishaji wa bidhaa za Kampuni ya Oryx Energies Tanzania Limited.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo Subira Mgalu amesema kamati hiyo inatambua mchango na uwekezaji uliofanywa na Oryx Energies ambapo katika kipindi cha miaka minne imechangia pato la taita Sh.trilioni 1.2 huku pia ikiwa imetoa ajira za moja kwa moja 1000 na kwa asilimia kubwa walioajiriwa ni vijana wa kitanzania.
“Katika uwepo wa miaka 25 ya Oryx Energies nchini imetoa mchango mkubwa katika kuwezesha Watanzania kupata ajira lakini pia imekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa la Tanzania.”
“Wabunge wamepata fursa ya kuona mambo mazuri kupitia kampuni hii ikiwemo maabara ya kisasa kwa ajili ya kupima ubora wa vilainishi lakini kwa upande wa ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia majumbani hivi sasa kumekuwepo na ongezeko kubwa la watumiaji kutoka asilimia sita ya awali hadi kufikia asilimia 26 na ongezeko hili linakchango mkubwa wa Oryx Gas na wadau wengine.”
Aidha katika nishati safi ya kupikia amesema kamati ya nishati inampongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwani ndio kinara wa nishati safi na amekuwa akihamasisha matumizi ya nishati hiyo na sasa anatambulika katika medani za kimataifa.
Pia Mgalu amesema kamati hiyo inaendelea kusisitiza uwekezaji wenye tija na unaoleta matokeo katika taifa letu lakini kubwa mchango wa kuinua uchumi wa nchi na watanzania kwa ujumla wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania Limited Imani Mtafya amesema kampuni hiyo imekuwepo kwa miaka 25 sasa na uwepo wake umetoa mchango mkubwa kwa Watanzania na hasa kuhakikisha wanapata bidhaa bora hasa ya vilainishi.-
Aidha amesema Oryx Energies kwa mwaka inachangia Sh.bilioni 300 ambayo ni sawa na asilimia 0.1 sambamba na kuwa na ajira asilimia 99 kwa watanzania .
Wakati huo huo Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoite Araman amewahakikishia wabunge wa kamati hiyo kuwa kampuni hiyo itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi zao katika kuiunga mkono Serikali ambayo imelenga ifikapo mwaka 2030 asilimia 80 ya Watanzania iwe inatumia nishati safi ya kupikia.














EmoticonEmoticon