NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Serikali imewataka wanamichezo na wadau wa sekta ya michezo nchini kutumia mfumo wa miliki ubunifu kulinda vipaji, majina na chapa zao ili kuongeza thamani ya kiuchumi ya shughuli zao na kujijengea maisha bora baada ya michezo.
Wito huo umetolewa Mei 8, 2026 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Salvio Kapinga wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu Duniani yaliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam jijini Dar es Salaam.
Waziri Kapinga alisema bado kuna haja kubwa kwa wanamichezo, vilabu na mashirikisho ya michezo nchini kuelewa na kutumia vyema mfumo wa miliki ubunifu katika kulinda haki zao za kibiashara na ubunifu.
Alisema matumizi sahihi ya miliki ubunifu yanaweza kusaidia wanamichezo kuongeza mapato kupitia matumizi ya majina, picha, nembo na chapa zao katika shughuli mbalimbali za kibiashara.
“Niwasihi viongozi wa vilabu vya michezo, mashirikisho na wadau wote wa michezo kuwasaidia wanamichezo katika vilabu na mashirikisho yenu kuhakikisha wanalinda haki zao ikiwemo matumizi ya picha au taswira zao katika bidhaa au biashara za watu wengine,” alisema Waziri Kapinga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA, Neema Mori alisema ni muhimu kwa wadau wa michezo kuhakikisha hawatumii alama za biashara au nembo zisizo zao bila ridhaa ya wamiliki halali.
Profesa Mori alisema matumizi ya alama zilizosajiliwa kinyume cha sheria yanaweza kusababisha migogoro ya kisheria na kuathiri maendeleo ya biashara na tasnia ya michezo kwa ujumla.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa aliwahimiza wanamichezo kutumia majina yao kama chapa za biashara zitakazowasaidia kuendelea kunufaika kiuchumi hata baada ya kustaafu michezo.
Alisema baadhi ya wanamichezo duniani wamefanikiwa kujenga thamani kubwa ya kifedha kupitia chapa zao binafsi, akitolea mfano chapa ya CR7 inayomilikiwa na Cristiano Ronaldo ambayo imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha mapato.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Leodigar Tenga alisema wakati taifa likielekea maandalizi ya mashindano ya 2027 Africa Cup of Nations, wadau wa michezo wanapaswa kuhakikisha bunifu zao zinalindwa dhidi ya wizi na matumizi yasiyo halali.
Alisema ulinzi wa chapa, alama na kazi za ubunifu utasaidia kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma zinazohusiana na michezo nchini.
Maadhimisho ya mwaka huu ya Miliki Ubunifu na utoaji wa tuzo kwa wadau wa michezo yamefanyika chini ya kauli mbiu isemayo, “Miliki Ubunifu na Michezo; Jitayarishe, Jipange, Vumbua.”
EmoticonEmoticon