BARAZA LA MAWAZIRI LA EAC KUKUTANA KWA DHARURA JIJINI ARUSHA

May 18, 2026





Maandalizi ya Mkutano wa 60 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), unaotarajiwa kufanyika tarehe 22 Mei 2026, yameanza rasmi kupitia vikao vya ngazi ya wataalamu vinavyoendelea kuanzia tarehe 18 hadi 20 Mei 2026 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha.

Kikao hicho cha wataalamu kimepokea na kujadilia taarifa ya Kamati ya Fedha na Utawala kuhusu masuala ya fedha ya Jumuiya, na rasimu ya bajeti ya Sekretarieti ya EAC pamoja na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Mapendekezo yatakayopitishwa katika ngazi hiyo yatawasilishwa kwa Makatibu Wakuu watakaokutana tarehe 21 Mei, 2026 kabla ya kuwasilishwa katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri utakaofanyika tarehe 22 Mei, 2026.



Vilevile, mkutano huo wa siku tano kuanzia tarehe 18 hadi 22 Mei, 2026 unalenga kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa maelekezo na maamuzi yaliyotolewa na Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi za EAC, hususan katika maeneo ya mipango na fedha

Baraza la Mawaziri la EAC ni chombo kikuu cha maamuzi na kusimamia shughuli za Jumuiya, katika hatua hii ya maandalizi ya bajeti, Baraza hilo lina jukumu la kupokea, kuchambua, kufanya marekebisho na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya Sekretarieti ya EAC kabla ya kuwasilishwa katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa rasmi.



Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unajumuisha wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ukionaongozwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Justin Kisoka.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »