WATENGENEZA MAUDHUI MTANDAONI WATAKIWA KUWA NGUVU YA KUBADILISHA JAMII KATIKA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

April 08, 2026




📌 Kupitia uelimishaji na uhamasishaji wa jamii


Katika mwendelezo wa mafunzo kwa watengeneza maudhui mtandaoni (Content Creators), awamu ya kwanza inayoendelea Jijini Arusha leo Aprili 8, 2026, Wizara ya Nishati imewahimiza washiriki kutumia majukwaa yao ya kidijitali kama chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.


Akitoa wito huo, Mhandisi Benezeth Kabunduguru kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia amesema watengeneza maudhui wana nafasi kubwa ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, pamoja na kuhamasisha jamii wanayoizunguka na wafuasi wao kubadili mitazamo na kuanza kutumia nishati hizo.

Akiwasilisha mada yake, Mhandisi Kabunduguru ameeleza kuwa watengeneza maudhui wanaweza kutumia mbinu mbalimbali zenye mvuto kama vile picha za video fupi, vichekesho, hadithi na simulizi za maisha halisi ili kufikisha ujumbe kwa ufanisi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, amesisitiza kuwa nishati safi ya kupikia si aina moja tu, bali ipo katika mfumo mbalimbali ikiwemo gesi, umeme, mkaa mbadala na nyinginezo, ambazo zimeidhinishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa salama kwa afya ya binadamu na rafiki kwa mazingira.

Katika hatua nyingine, alibainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara wa ajenda ya nishati safi ya kupikia barani Afrika. Hivyo amewataka watengeneza maudhui kumuunga mkono kwa vitendo ili kufanikisha lengo la kitaifa la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Ameongeza kuwa watengeneza maudhui wanapaswa kutumia ushawishi wao kubadilisha mitazamo hasi ya jamii kwa kutumia lugha sahihi, ubunifu na maudhui yenye kugusa maisha ya watu.

Kwa mujibu wa takwimu, takribani vifo 33,000 hutokea kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia. Hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kuifikisha elimu hii kwa wananchi wengi zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali yanayotumiwa na watengeneza maudhui.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, huku Wizara ya Nishati ikiwa miongoni mwa wadhamini wakuu.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »