ACHENI KUTANGAZA WATU,TANGAZENI NCHI-WAZIRI MAKONDA

April 30, 2026


Na Immaculate Makilika - MAELEZO

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda amewataka wadau wa sekta ya habari kubadili ajenda ya kutangaza watu badala yake watangaze fursa za uchumi zilizopo nchini.

Ametoa rai hiyo leo Aprili 30, 2026 katika Siku ya Tatu ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani iliyofanyika jijini Arusha.

“ Tuache ajenda ya kutangaza watu, tuitangaze nchi yetu. Tubadilishe mkakati kutoka ajenda ya kusifia watu, tuambieni fursa za uchumi zilizopo,” amesema Waziri Makonda

Ameongeza kuwa waandishi wa habari waache kasumba ya kuwaandika vizuri wala rushwa na watu wasio na sifa njema katika jamii, badala yake wafanye kazi zao kwa maslahi ya Taifa.

Ametolea mfano kuwa hakuna idadi ya kutosha ya waandishi wanaoandika kuhusu sekta ya utalii au kilimo kama wanaoandika kuhusu masula ya siasa.

Amezungumzia kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na kuwaasa waandishi wa habari kushiriki kikamilifu ili kufikia malengo yaliyowekwa huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa mchango wa Vvyombo vya Habari kwa maendeleo ya nchi.

Aidha, Waziri Makonda amewataka waandishi wa habari kujiridhisha na vyanzo vya taarifa za kabla ya kuzisambaza kwa umma ili kuepuka upotoshaji na migogoro.

Kuhusu mapendekezo yaliyotelewa na wadau wa sekta ya habari ya kuboresha utendaji wa sekta hiyo nchini, Mhe. Makonda amesema Serikali imeyapokea mapendekezo yote 15 na itayafanyia kazi kwa kushirikiana na wadau.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa amesema kuwa lengo la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ni kutathimi na kulinda hali ya uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Ameongeza kuwa kupitia Maadhimisho hayo Serikali itapata fursa ya kukutana na washirika wake wa maendeleo na asasi za kiraia kujadili masuala ya mabadiliko ya utendaji kazi katika sekta ya habari pamoja na kuwaendeleza watayarishaji wa maudhui.

Naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tech and Media Convergency (TMC) na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo kwa mwaka 2026, Bi. Asha Abinallah amesema kuwa kupitia Maadhimisho hayo wadau wameandaa mapendekezo kadhaa ikiwemo kuitaka Serikali kuharakisha uanzishwaji wa Mfuko wa Habari na kuandaa sera rafiki za kuvutia uwekezaji katika sekta ya habari.

Vilevile, wameitaka Serikali kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kuendelea kutimiza majukumu yake ikiwemo kuwajengea uwezo wanahabari katika matumizi ya akili unde.

















Share this

Related Posts

Previous
Next Post »