Na mwandishi wetu, Arusha.
Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga, amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwawezesha kiuchumi watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri, ikiwemo asilimia 2 inayotengwa mahsusi kwa kundi hilo.
Mhe. Nderiananga ametoa kauli hiyo leo Machi 01, 2026 Jijini Arusha alipokutana na watu wenye ulemavu ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake iliyoanza Wilaya ya Moshi-Kilimanjaro.
Naibu Waziri Nderiananga, amewapongeza watu wenye ulemavu wa Mkoa wa Arusha kwa nidhamu ya kurejesha mikopo kwa wakati na kuhimiza waliomaliza kurejesha waweze kuomba tena ili kupanua shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, ameelekeza kuwa 30% ya manunuzi ya umma kwenye Halmashauri zote za Jiji la Arusha ziende kwenye makundi haya maalum kama vile watu wenye ulemavu, “tunapotengeneza masoko tutenge maeneo maalumu kwaaajili ya watu wenye ulemavu, na nataka kuona miradi ya watu wenye ulemavu kuwa ni miradi ya kielelezo Nchini’’Mhe. Nderiananga amesema
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuwakwamua kiuchumi watu wenye ulemavu, na ameahidi kuandaa hafla kwaajili ya kuwapongeza wanufaika wa Mikopo ya 2% waliofanya vizuri ili iwe kama sehemu ya hamasa na kielelezo kwa wale ambao hawajafanyi vizuri na ambao wanatamani kupata mikopo hiyo.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya watu wenye ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu Bw. Kizito Wambura amesema Serikali inania thabiti ya kuleta mabadiliko kwa watu wenye ulemavu na kutatua changamoto zilizobainishwa kupitia mfumo wa kieletroniki wa taarifa za watu wenye ulemavu (PDMIS) ambao tunategemea ufike kwenye maeneo yote ya Tanzania.










EmoticonEmoticon