Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Prof. Said Aboud
📍8 Juni, 2026
Arusha
Takribani washiriki 450 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki katika Kongamano Kuu la 33 la Mwaka la Kisayansi la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) litakalofanyika jijini Arusha kuanzia Juni 9 hadi 11, 2026. Mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa (Mb.), Waziri wa Afya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Said Aboud, amesema kongamano hilo litawakutanisha watafiti, watunga sera, wataalamu wa afya, wanataaluma, wanafunzi pamoja na wadau wa maendeleo kwa lengo la kubadilishana maarifa na kujadili suluhisho za changamoto mbalimbali za afya nchini na kimataifa.
Amesema mada kuu ya kongamano hilo ni "Huduma za Afya kwa Wote: Kujenga Mfumo Madhubuti na Endelevu wa Afya kwa Tanzania ya 2050", mada inayodhihirisha dhamira ya taifa ya kuimarisha mfumo wa afya unaotegemea ushahidi wa kisayansi, ubunifu na matumizi ya matokeo ya utafiti katika maamuzi ya sera na utekelezaji.
Kwa mujibu wa Prof. Aboud, kongamano hilo limepokea jumla ya mawasilisho 339 ya kisayansi. Kati ya hayo, mawasilisho nane yatatolewa kwa njia ya mdomo huku symposia sita zikitoa jukwaa la majadiliano ya kitaalamu kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
Aidha, kongamano hilo litajumuisha maonesho ya tafiti na ubunifu kutoka NIMR na taasisi mbalimbali, majadiliano ya kisera pamoja na fursa za kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao ya kitaalamu miongoni mwa wadau wa sekta ya afya.
Prof. Aboud amesema matokeo yanayotarajiwa kutokana na kongamano hilo ni pamoja na kuimarisha matumizi ya matokeo ya utafiti katika maamuzi ya kisera, kupendekeza mikakati ya kuboresha huduma za afya, kutambua maeneo mapya ya vipaumbele vya utafiti, kuongeza ushirikiano kati ya serikali, watafiti na wadau wa maendeleo, pamoja na kuimarisha mchango wa Tanzania katika tafiti za afya kikanda na kimataifa.
Ameongeza kuwa kongamano hilo litatoa fursa ya kuonesha namna tafiti na ubunifu vinavyoweza kuchangia katika kujenga mfumo wa afya wenye uimara, usawa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo.
Pia amevishukuru vyombo vya habari kwa ushirikiano wake na NIMR katika kuhabarisha umma kuhusu matokeo ya tafiti na maendeleo ya kisayansi, huku akivihimiza kuendelea kuripoti kwa usahihi, uwazi na weledi ili kuhakikisha ushahidi wa kisayansi unawafikia wananchi.
"NIMR itaendelea kuwa mhimili wa taifa katika uzalishaji na matumizi ya ushahidi wa kisayansi unaoongoza maamuzi ya afya na maendeleo, kuhakikisha utafiti unatafsiriwa moja kwa moja kuwa suluhisho kwa wananchi," amesema Prof. Aboud.
#WizaraYaAfya#NIMR#UtafitiKwaAfyaBora#AJSC2026#

EmoticonEmoticon