Na Oscar Assenga,TANGA
Zaidi ya wananchi 20,000 kutoka kaya masikini mkoani Tanga wameanza kunufaika na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa kaya zenye kipato cha chini.
Mpango huo, unaotekelezwa kwa awamu ya kwanza na ya pili, unalenga kuwafikia wananchi walio katika mazingira magumu kiuchumi ili kuwawezesha kupata huduma za afya bila kikwazo cha gharama za matibabu. Ufadhili wa mpango huo unatolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ukiwa na lengo la kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa kaya masikini.
Hadi sasa, zaidi ya wanufaika 20,000 kutoka kaya 7,816 wamepatiwa kadi za bima ya afya na wameanza kutumia huduma hizo tangu Machi mwaka huu. Hatua hiyo imeelezwa kuwa imeleta matumaini mapya kwa wananchi wengi ambao hapo awali walikabiliwa na changamoto ya kumudu gharama za matibabu.
Akizungumza katika Maonesho ya Kibiashara ya Mwahako, Daktari Lawi Kupaza kutoka Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Tanga amesema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, huku wengi wa walengwa waliostahili tayari wakikabidhiwa kadi zao.
Amesema zoezi hilo linaendelea vizuri katika halmashauri zote za mkoa huo, huku awamu ya pili ikitarajiwa kufikia kaya nyingine 1,300.
“Kwa sasa tunaendelea na ugawaji wa kadi pamoja na uhakiki wa taarifa za wanufaika. Tunawahamasisha wananchi kujitokeza kuhakiki taarifa zao ili waweze kupata huduma kwa wakati,” amesema Dkt. Kupaza.
Hata hivyo, amekiri kuwepo kwa changamoto ya kuwafikia wanufaika wote kwa wakati kutokana na ukubwa wa maeneo ya utekelezaji na ratiba za shughuli mbalimbali.
“Kuna changamoto ya kuwafikia wanufaika wote kwa wakati kutokana na ratiba na ukubwa wa eneo la utekelezaji. Hata hivyo, watendaji wa kata na vijiji wanaendelea kusaidia katika uhamasishaji,” ameongeza.
Kwa upande wake, Afisa Madai wa NHIF, Neema Kisinga, ameitaka jamii kuendelea kujiunga na bima ya afya ili kujikinga na gharama kubwa za matibabu.
Amesema mfuko huo una vifurushi mbalimbali vinavyowezesha wananchi kupata huduma za afya kwa gharama nafuu, ikiwemo kifurushi cha Tarangire ambacho kinatoa huduma za matibabu, vipimo na ushauri wa daktari kwa gharama nafuu kwa mwaka mzima.
“Kuwa na bima ya afya kunapunguza mzigo wa kulipia huduma kila unapougua au kuhitaji matibabu. Hii ni njia bora ya kujilinda na gharama zisizotarajiwa za afya,” amesema Kisinga.
Mpango huo unaendelea kuonekana kama hatua muhimu katika juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wote, hususan wa kipato cha chini, wanapata huduma bora za afya bila kuathiriwa na changamoto za kifedha.
.jpg)



EmoticonEmoticon