Ushirikiano wa Oryx Gas Tanzania na Doris Mollel Foundation Waimarisha Afya na Mazingira Kwimba

March 01, 2026
WATUMISHI wa sekta ya afya katika Wilaya ya Kwimba wamepatiwa nishati safi ya kupikia ya mitungi mikubwa ya gesi ya Oryx na majiko yake pamoja na kupatiwa elimu ya matumizi sahihi na salama ya nishati hiyo.

Mitungi hiyo ya gesi ya Oryx kwa watumishi hao wa sekta ya afya Wilaya ya Kwimba Februari wamepatiwa jana Februari 28,2026 wakati wa uzinduzi wa jengo la kisasa la kuhudumia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) katika Wilaya hiyo na jengo hilo ya limejengwa kwa ufadhili wa Doris Mollel Foundation (DMF) kwa kushirikiana na Keep a Child Alive (KCA)

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman ,Meneja Mafunzo wa kampuni hiyo Peter Ndomba amesema wamegawa mitungi ya gesi kwa watumishi hao wa hospitali Wilaya ya Kwimba kama sehemu ya kuunga mkono jitihada hizo za kuhudumia watoto njiti lakini pia kuendelea kuhamasisha nishati safi ya kupikia nchini kwa kundi hilo muhimu.

“Oryx Gas Tanzania pamoja na Doris Mollel Foundation tayari tuna mkataba wa miaka minne katika kuunga mkono juhudi zake kwa mtoto njiti na leo tunatoa mitungi 167 kwa wafanyakazi wote wa idara ya afya hapa Kwimba

“Unajua kwanini tunafanya hivyo?Tunajua watu wa idara ya afya ndio wanakutana na wagonjwa kwa mara ya kwanza,wao ndio wasomi na ndio watalaam ambao wanaweza kuelekeza wagonjwa jinsi gani ya kujiepusha na madhara ya kuni na mkaa.

“Hivyo tumeona ni muhimu kundi hili kulisapoti na kupitia ubia wetu sisi na Dorris Mollel Foundation tutaendelea kufanyakazi ndani ya miaka minne ili kwa pamoja tujue tumefikia hatua gani kwa nchi nzima,”amesema Ndomba .

Kuhusu mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya nishati ya kupikia ya gesi ,Ndomba amesema Oryx Gas lengo pia ni kuiwezesha kada hiyo ya sekta ya afya kuwa na uelewa mpana kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ya gesi kisha wawe mabalozi kwa wananchi wengine wakiwemo wagonjwa.

“Tumeamua kutoa mafunzo haya kwasababu tunajua wananchi wanapopata matatizo ya kiafya wanakuja hospitali kwahiyo wale ndio wanakuwa watu wa kwanza kukutana na wananchi wenye matatizo.

“Tunafurahi mwitikio ni mkubwa na mafunzo haya ni mwanzo tu kwani tutakwenda katika taasisi zote,shule mbalimbali na kila jukwaa tutaweza kufika ili sasa muendelezo mzima wa matumizi ya nishati safi uweze kufikia watu wote”

Kwa upande wao watumishi wa sekta ya afya katika Wilaya hiyo wameishukuru kwa kupatiwa mitungi ya gesi pamoja na elimu ya matumizi sahihi na salama ya gesi ya kupikia kwani wanaamini watakuwa mabalozi waziri wa kuelezea faida za kutumia nishati hiyo ya kupikia ambayo ni salama kiafya.

Akizungumza baada ya kupatiwa mitungi hiyo Dk.Makore Maro ameishukuru kampuni hiyo kwa kuwapatia mitungi ya gesi ambayo kwao itakuwa na tija kubwa huku wakieleza kwa sasa kupitia majiko ya gesi waliyopatiwa watatumia muda mfupi kuandaa chakula na hivyo kuwa na muda mwingi wa kuhudumia wagonjwa.

Pia amesema mitungi hiyo itasaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya kutumia kuni na mkaa huku akisisitiza wataendelea kuwaelimisha wananchi katika maeneo tunayoishi ili waondokane na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanaleta uharibifu wa mazingira.

Wakati huo huo Maria Sakimu ambaye ni Muuguzi na Msimamizi Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba amesema wanashukuru kupatiwa nishati safi ya kupikia huku akieleza watakuwa mabalozi kwa wengine kuelezea umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia ya badala ya kutumia nishati chafu ya kupikia ya kuni na mkaa .

Kwa upande wake Christian Mvula ambaye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba amesema wanashukuru Oryx kwa kuwapatia mafunzo ya matumizi sahihi ya gesi sambamba na kuachana na mkaa na kuni na kuingia katika matumizi ya gesi.

“Tumapatiwa mitungi mikubwa ya gesi na majiko yake lakini pamoja na elimu sahihi ya kutumia gesi ya kupikia.Watumishi sekta ya afya tunafurahi kupata huduma hiyo na kimsingi tulikuwa tunateseka kutumia kuni na mkaa ambayo wakati mwingine ni ngumu kupatikana hasa kipindi hiki cha mvua.

“Sasa tumeelewa matumizi ya gesi iliyosalama kama nishati ya kupikia na kwetu imekuwa nafuu kwani awali tulikuwa na uelewa tofauti, kulikuwa na nadharia nyingi mtaani kuhusu gesi ikiwemo usalama na gharama.”

Wakati huo huo Ofisa Muuguzi Salome Malale amesema ametumia gesi kwa miaka 15 lakini hakujua faida na hasara za gesi na yeye kama muuguzi kuna changamoto nyingi zimetokea kwa mfano jamii nyingi zinatumia kuni na mkaa.

“Ninavyojua walikuwa wanapata matatizo ya mapafu wengine macho na walikuwa wanakuja kutibiwa hospitalini, sasa kwa elimu ambayo nimeipata naweza kutoa elimu kwa jamii kutumia gesi na tuachane kutumia kuni au mkaa.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »