UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU YA UMEME UTAIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME KWA WANANCHI- WAZIRI NDEJEMBI

January 06, 2026



📌 *Awahimiza Wananchi kulinda miundombinu ya umeme*


📌 *Wakandarasi waelekezwa kukamilisha miradi ya umeme kwa wakati*


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya umeme nchini kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na wa kuaminika.


Mhe. Ndejembi ameyasema hayo Januari 06, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua vituo vya kupokea na kupoza umeme vya Gongolamboto, Kinyerezi, Mabibo na Ubungo.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 280 katika utekelezaji wa miradi ya vituo vya kupokea na kupoza umeme pamoja na njia za kusafirisha umeme, ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa matumizi ya majumbani na viwandani, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa viwanda.


Ameeleza kuwa Jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa maeneo yanayotumia umeme kwa kiwango kikubwa zaidi nchini, likitumia wastani wa megawati 750, huku Mkoa wa Pwani ukitumia wastani wa megawati 100, hususan katika shughuli za viwanda. Kwa pamoja, mikoa hiyo hutumia zaidi ya megawati 800, hali inayodhihirisha umuhimu wa uwekezaji unaofanywa katika kuboresha miundombinu ya umeme.

Aidha, Mhe. Ndejembi amebainisha kuwa Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Gongolamboto kinafanyiwa maboresho kwa kubadilisha transfoma ya awali yenye uwezo wa MVA 50 na kuweka transfoma yenye uwezo mkubwa zaidi. Ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika Julai 2026 na utaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wakazi wa Gongolamboto, Mbagala, Kigamboni na maeneo ya jirani, ambayo yanategemea umeme kwa shughuli za viwanda na biashara.

Vilevile, ameeleza kuwa Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mabibo kinatarajiwa kukamilika Agosti 2026, na kitachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Jiji la Dar es Salaam.

Amewahimiza wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati uliopangwa, akisisitiza kuwa wananchi wanategemea huduma hizo muhimu. Pia amewataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya umeme, akieleza kuwa fedha nyingi za Serikali zimewekeza katika miradi hiyo kwa lengo la kuhakikisha umeme unapatikana muda wote.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, amesema kuwa TANESCO inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha miradi yote inayolenga kuondoa changamoto za usafirishaji na upatikanaji wa umeme inakamilika kwa wakati.


Ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 15 katika miradi ya umeme inayoendelea kutekelezwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma kutokana na ongezeko la uwekezaji na idadi ya watu. Amesisitiza kuwa sekta ya umeme ni sekta wezeshi kwa maendeleo ya Taifa.


Bw. Twange ameongeza kuwa kukamilika kwa Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mabibo kutaongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka vituo vya uzalishaji vya Kinyerezi na Bwawa la Umeme la Julius Nyerere kupitia Kituo cha Chalinze, hatua itakayopunguza mzigo katika Kituo cha Ubungo, kupunguza utegemezi, na kuongeza kiasi cha umeme kinachowafikia wateja wa Gongolamboto, Mbagala na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Taifa kwa ujumla.


#NishatiTupoKazini

#TanzaniaYetuSote

#NchiYetuKwanza

#MaendeleoEndelevu

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »