TUME YASISITIZA ELIMU YA LOCAL CONTENT NA UTEKELEZAJI WA CSR

November 20, 2025




_Ajira za Migodini Zafikia 19,874, Watanzania Wafanya Kazi kwa Asilimia 97.5_


DODOMA 


Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, ametoa wito kwa Waratibu wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) na CSR katika mikoa kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na rasilimali za madini.

Akizungumza leo Novemba 20, 2025 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa waratibu hao, Mhandisi Lwamo amesema ni muhimu kusimamia kwa umakini Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini pamoja na Wajibu wa Wamiliki wa Leseni kwa Jamii (CSR) ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini na sekta nyingine zinazohusiana.

“Elimu kwa wananchi ni nguzo muhimu ya kuwawezesha kuchangamkia fursa za ajira na biashara migodini, hususan baada ya Tume kutangaza orodha ya bidhaa na huduma zinazopaswa kutolewa na kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100,” amesema Mhandisi Lwamo.

Aidha, amewataka waratibu kuwa kiungo madhubuti kati ya Makao Makuu ya Tume ya Madini na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa katika kuhakikisha usimamizi wa Local Content na CSR unatekelezwa ipasavyo.

Mhandisi Lwamo ameongeza kuwa sekta ya madini inaendelea kukua kwa kasi, huku mchango wake katika Pato la Taifa ukifikia asilimia 10 kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Annasia Kwayu, amesema Tume itaendelea kusimamia kikamilifu ushirikishwaji wa Watanzania katika maeneo yote ya sekta hiyo, ikiwemo ajira na manunuzi ya migodi. 


Amebainisha kuwa hadi sasa sekta imezalisha jumla ya ajira 19,874, ambapo asilimia 97.5 ni Watanzania na asilimia 2.5 pekee ni wageni.


Kuhusu manunuzi, Kwayu amesema kuwa mwaka 2024 migodi ilinunua bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 2.03, huku kampuni za Kitanzania zikichangia Dola za Marekani Bilioni 1.79, sawa na asilimia 88 ya manunuzi yote kiashiria cha mafanikio katika utekelezaji wa Local Content.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »