Tanzania na Oman zimeendelea kuonyesha dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kazi na ajira ili kuongeza ajira zenye staha, kulinda haki za wafanyakazi na kukuza uchumi wa mataifa yote mawili.
Hayo yamebainishwa wakati wa kikao cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu na Waziri wa Kazi wa Oman, Dkt. Mahad bin Said bin Ali Baawain walipokutana katika Mkutano wa Mawaziri wa Kazi Duniani (Global Labour Market Conference) uliofanyika Jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Aidha, katika kikao hicho Waziri Sangu alielezea umuhimu wa kukamilishwa na kutiwa saini kwa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa masuala ya Kazi na Ajira (MoU) kati ya nchi hizo mbili, ili kuweka mfumo rasmi na endelevu wa usimamizi wa masuala ya ajira, ulinzi wa haki za wafanyakazi na utatuzi wa changamoto za kiutendaji zinazojitokeza.
Vilevile, Waziri Sangu ameishukuru Serikali ya Oman kwa kuendelea kutoa fursa za ajira kwa Watanzania katika sekta mbalimbali. Pia, amesema idadi ya Watanzania wanaofanya kazi nchini Oman imeendelea kuongezeka , jambo linaloonesha kuimarika kwa mahusiano ya ajira kati ya mataifa hayo mawili.
Kwa upande mwingine, nchi hizo zimekubaliana kuendeleza ushirikiano kwa kuendelea kupanua wigo wa ajira zenye staha, kulinda haki za wafanyakazi na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kijamii kati ya mataifa yetu mawili.
EmoticonEmoticon