Na Mwandishi Wetu, Arusha.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeonyesha dhamira ya dhati Kufanya kazi bega kwa bega na wadau wa maendeleo kuhakikisha uboreshaji wa mfumo wa usimamizi wa mafunzo endelevu wa walimu kazini yaani MEWAKA unaboreshwa na kukamilika kwa wakati na kwa ufanisi ili kuwezesha mahitaji ya walimu wa Sekondari.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha warsha iliyofanyika kwa muda ya siku mbili ya tarehe 28 na 29 Agosti 2025, ya mapitio ya mfumo wa MEWAKA ulioboreshwa Mratibu wa Mradi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Lina Rujweka, alitoa shukrani kwa juhudi na muda uliowekezwa na wadau wote, ikitambua mchango wao muhimu unaotarajiwa kuleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mradi huu hasa UNESCO na Jamhuri ya Korea kupitia mradi wa ‘’KFIT III wa Transforming Education through ICT in Africa’’ kwa kuendelea kutoa msaada wa kifedha.
Shirika la UNESCO Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), inaendelea na juhudi za uboreshaji mfumo wa MEWAKA ili kuzingatia mahitaji ya walimu wa shule za sekondari.
Ushirikiano huu ulitokana na tathmini ya mahitaji iliyoonyesha kuwa mfumo wa sasa ulikuwa umeundwa mahsusi kwa ajili ya kuwa jukwaa la mafunzo ya maendeleo ya kitaaluma kwa walimu wa shule za msingi.
Hivyo, wadau walikutanishwa ili kupitia toleo la awali la mfumo wa MEWAKA kwa lengo la kuhakikisha umuhimu, ubora, na uendelevu wa muda mrefu wa jukwaa hilo.
Wadau hao walikuwa kutoka wizara ya elimu, sayansi na Teknolojia , Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Taasisi ya Elimu Tanzania, Tume ya Kitaifa ya UNESCO na baadhi ya walimu wa shule za sekondari.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ally Mape alisema majukwaa ya kidijitali ni nyenzo yenye nguvu ya maendeleo ya kitaaluma, yanayochangia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha walimu kupata ujuzi na kujiamini ili kufanikisha kazi zao katika Dunia ya sasa.
Kwa upande wake mkuu wa Sekta ya Elimu kutoka Ofisi ya UNESCO Dar es Salaam, Dkt. Faith Shayo, ameeleza kuwa lengo kuu ni kupanua upatikanaji wa mafunzo endelevu ya kitaaluma kupitia majukwaa ya kidijitali, hivyo itasaidia kuboresha matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji kote nchini.
Hata hivyo Dkt. Shayo aliwahimiza wadau kutoa maoni na mitazamo yao kusaidia kuhakikisha toleo la mwisho la mfumo huu sio tu kuwa la kisasa bali pia rahisi kutumia na lenye matokeo chanya.
Mpango huu unalingana na juhudi za Serikali za kuunganisha TEHAMA katika elimu, kama inavyoonekana katika sera na mikakati muhimu ya kitaifa ikiwemo Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023, Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Kidijitali 2025 – 2030, Dira ya Maendeleo ya 2050, Mitaala ya Elimu ya Msingi na ya Ualimu, pamoja na mipango ya kimataifa kama vile Malengo ya Maendeleo Endelevu hasa lengo namba nne.
EmoticonEmoticon