SIWEZI KUISUSA CCM,NITASHIRIKI KUTAFUTA KURA ZA WAGOMBEA -UMMY

September 07, 2025


Na MASHAKA MHANDO, Tanga

ALIYEKUWA mbunge wa Jimbo la Tanga, Ummy Mwalimu, amesema hawezi kukisusa Chama Cha Mapinduzi (CCM) badala yake atahakikisha anashirikiana na walioteuliwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili waweze kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni wa Chama hicho wa kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Tanga, uliofanyika katika uwanja wa Vijana uliopo kata ya Duga, Ummy alisema CCM imemlea na kisha kumpa Uwaziri kwa miaka 14 hivyo, hawezi kuisusa wala kufanya nongwa.

"Roho yangu ni nyeupe, heshima niliyopewa na CCM kuwa mbunge kwa miaka 15, Waziri miaka 14, nikifanya hasira nitakuwa namkufuru Mungu, nawaomba sana mchagueni Kassim Mbaraka Makubel awe mbunge wa Tanga," alisema.

Ummy alisema kuwa Tanga itaendelea kuwa Fahari yake kwavile ni nyumbani hivyo hawezi kususa na ataendelea kutafuta kura za mgombea Urais wa Chama hicho, mbunge na madiwani katika Jiji la Tanga.

Alisema hakuwa akijulikana lakini heshima aliyopewa na CCM katika kipindi chote amelelewa na kuimarishwa katika uongozi hivyo anaheshimu maamuzi ya Chama na atakipigania kuhakikisha wagombea wote wanashinda katika uchaguzi.


Aliwaomba wananchi wa Jiji la Tanga wasifanye makosa kura zote wampe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amemuelezea kama kiongozi anayeguswa na changamoto zinazowakabili Watanzania.



"Ndugu zangu nilipata heshima ya kufanya kazi na Marais watatu, Rais Samia ni mama wa kipekee, mama anayejali na kuumizwa na changamoto za Tanzania, tusifanye makosa kura zote Wana-Tanga tumpe na wagombea wa CCM," alisema Ummy.


Alisema kabla ya kwenda kwenye mkutano huo, alikutana na kuteta na mgombea ubunge wa Jimbo la Tanga, Makubel ambaye amemuahidi kumpa ushirikiano mkubwa wakati wa kampeni na baada ya kuwa mbunge kwa ajili ya maslahi mapana ya watu wa Tanga.


Mjumbe wa Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM na Katibu Mstaafu wa UWT, Halima Mamuya aliwataka wananchi wa Tanga wawe wamoja na wakipigania chama hicho kiweze kushinda na wawapigie kura wagombea wa CCM Oktoba 29 mwaka huu.


"Hivi vijinenoneno hayakuwa maneno ilikuwa ni fitina, nitakwenda kumwambia mwenyekiti wetu kuwa Tanga ni Moja na watakipigia kura chama Cha Mapinduzi," alisema.


Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga na mjumbe wa Kamati Kuu Rajab Abdallah aliwataka wananchi wa mkoa wa Tanga kuhakikisha wanawachagua wagombea wa CCM kwavile imetekelezwa ilani yake vizuri na imekuja na ilani nyingine ambayo pia imeweka vipau mbele vingi ikiwemo miradi ya maendeleo.


Alisema yaliyofanywa na Rais Dkt Samia katika mkoa wa Tanga wananchi wameona na hawana sababu ya kupoteza kura kwa chama hicho kwavile hakuna chama kingine chenye dhamira ya kuwaongoza Watanzania Bali ni CCM.


"Hakuna chama kingine cha siasa chenue dhamira ya kutaka kuwaongoza Watanzania, CCM bado Ina nguvu na Ari kubwa ya kuwaongoza Watanzania wapeni kura wagombea wetu," alisema.


Alisema Rais Samia anaomba kura kwasababu ametekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 kama walivyoahidi.


Mgombea ubunge wa Jimbo la Tanga Kassim Amari Mbaraka maarufu Makubel aliwasomea ilani ya CCM ya mwaka 2025-20230 wananchi waliokuwanyika katika mkutano huo ambapo alisema miongoni mwa litakalotekelezwa ni usanifu wa kujengwa daraja la juu kutoka Kwaminchi hadi ofisi ya Mkuu wa mkoa.


Pia alisema kutajengwa ofisi sita za serikali za mitaa, ujenzi wa zahanati, Majengo ya watumishi lakini pia kuboresha huduma za afya.

Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »