Taasisi ya ALII, HakiElimu Waandaa Viongozi wa Kesho Kupitia NEXT GEN

September 08, 2025
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

TAASISI ya ALII – Africa Leadership Initiative for Impact kwa kushirikiana na HakiElimu imezindua rasmi Jukwaa la Kuwajengea Uwezo wa Uongozi Vijana (NEXT GEN) kwa vijana 100 waliohitimu kidato cha sita kutoka shule mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo leo Septemba 8, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shirikia la The African Leadership Initiatives For Impact, Joseph Malekela amesema lengo ni kuongeza ufanisi wa kiuongozi hususan kwa vijana watakaoshika nyadhifa mbalimbali na hivyo kuongeza mchango wao katika maendeleo endelevu nchini.

Amesema kuwa vijana wengi hawapati nafasi ya kushauriwa, kujifunza uongozi, au kushiriki kwenye meza ya maamuzi hivyo kupitia mafunzo hayo vijana wanakuwa na ujuzi na uwezo wa kuleta mabadiliko katika jamii na taifa.

Aidha amesema mafunzo hayo yatawawezesha kutambua sera na mifumo hivyo kuwa na mwelekeo wenye tija kwa jamii.

Amesema viongozi hubeba maono na mwelekeo wa familia, taasisi, jamii au taifa lolote. Kwa sababu hiyo, jukwaa hilo la kujenga viongozi ni muhimu kwa vijana wenyewe na taifa kwa ujumla.

"Tunafahamu, kuna majukwaa mengine mengi yanayofanya kazi ya namna hii, zikiwemo shule ambako vijana hawa wametoka. Hata hivyo jukwaa hili linaleta upekee wa aina yake kwa kuvitambua vipaji vya Uongozi". Amesema

Kwa upande wake Meneja wa Idara ya Utafiti, Ubunifu na Uchambuzi wa Sera wa HakiElimu Mwemezi Makumba amesema kuwa kwa takribani miaka 23 sasa, HakiElimu imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha uzalishaji wa raia wenye fikra makini na mchango chanya kwa taifa lao kupitia elimu.

"Wengi mnatufahamu kwa matangazo yetu yanayohusu uboreshaji wa elimu, lakini pia tunatoa mchango mkubwa katika kuboresha sera za elimu, mitaala na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika elimu". Amesema

Aidha Makumba amewapongeza wazazi na walezi wa watoto hao, pamoja na washirika na wafadhili wakiwemo Serikali ya Ireland kupitia IDP, Norwegian Church Aid, Ubalozi wa Marekani Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na taasisi mbalimbali za umma na asasi za kiraia katika kuhakikisha wanafanikisha jambo hilo.

Amesema kuwa vijana, hao kama sehemu ya kwanza ya programu hiyo ambayo itakuwa na mwendelezo, kuzingatia mafunzo na kuyaishi katika kila ngazi ya maisha yao.

"Tunatarajia kuziona nyota zenu za uongozi ziking’aa vyuoni, katika biashara, mashambani, na makazini mtakakokwenda hapo baadaye. Ni bahati iliyoje kwamba programu hii itakuwa nanyi katika safari hii na kuendelea kuwaongoza.

Pamoja na hayo amewasihi kuwa mabalozi wazuri wa jukwaa hilo na kama ilivyo kwa vijana hao wa ALII, watakuwa sehemu ya wanafunzi wa zamani (Alumni) wa NEXT GEN na watachangia katika kuzalisha na kuwalea vijana wenzetu watakaokuja nyuma yao hata baadaye.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Suleiman Mvunye ambaye ndiye aliyefungua Mafunzo hayo, amewataka vijana kujijenga katika misingi ya uadilifu na uzalendo ili kutengeneza kizazi cha viongozi watakaoweka mbele maslahi ya taifa na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »