SERIKALI YAPANIA KUANDAA WALIMU USHIRIKIANO WA ATE NA WIZARA WAZAA MATUNDA KWA WATAFUTA AJIRA

September 25, 2025

 

KATIKA  kuhakikisha mafunzo ya darasani yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amekutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bi. Suzzane Ndomba, kwa mazungumzo ya namna ya kuwawezesha vijana wahitimu kupata mafunzo ya vitendo sehemu za kazi.

Mkutano huo umefanyika  katika ofisi za ATE jijini Dar es Salaam, ambapo Prof. Nombo alisema Serikali imefanya mapitio ya Sera ya Elimu na kuboresha mitaala ya ngazi zote ili vijana wapate ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Aidha, Prof. Nombo alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa walimu walioko kazini ili kuboresha mbinu za ufundishaji, akieleza kuwa ufundishaji bora ndio msingi wa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa maisha na ajira.

“Lengo la ziara hii ni kujadiliana na ATE kuhusu njia bora za kuwashirikisha waajiri katika kusaidia vijana waliopo vyuoni au waliomaliza masomo kupata mafunzo ya vitendo sehemu za kazi,” alisema Prof. Nombo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bi. Suzzane Ndomba, alisema ATE imekuwa ikisaidia wanafunzi kupata mafunzo kwa vitendo kupitia wanachama wake, wakiwemo viwanda na makampuni. Alitolea mfano wa Mradi wa Kukuza Ujuzi wa Vijana unaotekelezwa na ATE, uliowawezesha zaidi ya vijana 1,000 waliomaliza kidato cha nne kupata mafunzo ya miezi sita katika vyuo vya ufundi kabla ya kupelekwa makampuni kwa mafunzo ya vitendo, ambapo baadhi yao walipata ajira.

Aidha, alitoa wito kwa Watanzania kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kujifunza ujuzi kwa gharama nafuu bila kujali kiwango cha elimu rasmi walichonacho.

Mazungumzo hayo yameonesha dhamira ya pamoja ya Serikali na sekta binafsi katika kuimarisha ujuzi wa vijana na kuandaa nguvu kazi yenye mchango katika maendeleo ya taifa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »