
Na Augusta Njoji, Handeni TC
HALMASHAURI ya Mji Handeni, mkoani Tanga, imejipanga kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya wananchi, baada ya zahanati tatu mpya kukamilika na kutarajiwa kuanza kutoa huduma mwezi Oktoba mwaka huu.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Maryam Ukwaju, amesema ujenzi wa zahanati hizo umefanikishwa na serikali kwa kushirikiana na wananchi kupitia utaratibu wa uhamasishaji wa kuchangia maendeleo ili kusogeza huduma karibu na jamii.
Amesema tayari ameagiza Mganga Mkuu wa Halmashauri, Dkt. Hudi Muradi, kuhakikisha Mfumo Madhubuti wa Usimamizi na Uendeshaji wa Vituo vya Afya (GoTHOMIS) unasimikwa kabla ya vituo kuanza kutoa huduma.
Kwa upande wake, Dkt. Hudi ametaja zahanati hizo kuwa ni Bangu, Mankinda na Kwedigongo, ambazo kwa sasa zipo hatua za mwisho za ukamilishaji ikiwemo ujenzi wa vyoo na uwekaji wa vifaa tiba.
Ameeleza kuwa ujenzi wa Zahanati ya Bangu umegharimu Sh. milioni 83.4, Mankinda Sh. milioni 78, na Kwedigongo Sh. milioni 83.6, ambapo fedha hizo zimetokana na michango ya wananchi, fedha kutoka Serikali Kuu na Mapato ya ndani ya Halmashauri.
“Zahanati mpya ya Mankinda, ikianza kutoa huduma, itaongeza upatikanaji wa huduma za afya katika Kata ya Konje ambayo ilikuwa na zahanati moja pekee ikihudumia wakazi 12,750 wa mitaa mitano,” amesema.
Nao, baadhi ya wananchi wameishukuru serikali kwa kukamilisha ujenzi wa zahanati hioz na kudai kuwa itawaondolea kero ya kusafiri kati ya kilomita tano hadi sita kufuata matibabu, na badala yake sasa huduma zitapatikana jirani na maeneo yao.
EmoticonEmoticon