Mtandao wa Bloga Tanzania (TBN) umekemea vikali tabia inayoshamiri ya watu kujinadi kufanya utabiri kwa watu na taifa kupitia mitandao ya kijamii, ukisema vitendo hivyo vinakiuka Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Kauli hiyo imetolewa kama azimio katika kikao kazi cha mafunzo ya mabloga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Mabloga hao wameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kushirikiana kuwasaka na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaohusika na vitendo hivyo.
Katika kikao hicho, mabloga walibainisha kuwa kumeibuka kundi la watu wanaodai kuwa ni manabii na kutoa kauli zinazokiuka sheria za nchi na kuleta taharuki kuelekea uchaguzi. Walisisitiza kuwa baada ya kuchambua Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Act), walibaini kwamba 'utabiri' wa namna hiyo unavuruga haki ya msingi ya faragha ya wahusika.
Kwa mujibu wa Bw. Innocent Mungy, mtoa mada kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), sheria hiyo inakataza mtu kuzungumziwa kuhusu afya yake, mwenendo, au taarifa zake binafsi kutolewa bila ridhaa yake. Mungy alisisitiza kuwa sheria hii ina adhabu kali na lazima ifuatwe na kila mtu, si tu mabloga na waandishi wa habari.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na TCRA, yalilenga kuwaandaa mabloga kuripoti habari za uchaguzi kwa weledi na uadilifu.
Pamoja na mada ya ulinzi wa taarifa binafsi, mada nyingine muhimu zilizotolewa ni pamoja na Mwongozo wa Waandishi wa Habari katika Uchaguzi na Matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika uandishi wa habari.
Lengo kuu la mafunzo haya ni kuongeza uwezo wa mabloga kuhakikisha wanafuata sheria na maadili ya uandishi, jambo linalotazamiwa kuchangia mazingira ya uchaguzi yenye amani na utulivu.
@@@@@@@@@@@@@
EmoticonEmoticon