Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), - Innocent Mungi akitoa mada kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi.
Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, akiwasilisha mada katika mafunzo maalumu kuelekea uchaguzi mkuu mahususi kwa bloga yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Agosti 11, 2025 Jijini Dar es Salaam.
PDPC Yataka Mabloga Kulinda Taarifa Binafsi Uchaguzi 2025
Na Mwandishi Wetu.
DAR ES SALAAM, Agosti 11, 2025 – Waandishi wa habari na mabloga wametakiwa kuelimisha jamii kuhusu sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, ili kuzuia uvunjifu wa faragha na kuepusha madhara ya kisheria.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Innocent Mungy, wakati wa mafunzo maalum kuelekea Uchaguzi Mkuu, yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ombi la Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN).
Mungy alisema mabloga wana nafasi kubwa ya kuelimisha umma kuhusu sheria hiyo, hasa katika kipindi cha uchaguzi, na kuwaonya kuepuka kuchapisha taarifa binafsi za watu au wagombea.
“Ni kosa kisheria kuingilia mambo binafsi ya watu, na adhabu yake ni kali. Bloga mna wajibu wa kulinda faragha na kuepuka taarifa zinazoweza kuvunja sheria,” alisema Mungy.
Alibainisha kuwa maendeleo ya teknolojia yameongeza fursa na changamoto katika uandishi, hivyo mabloga wanapaswa kutumia majukwaa yao kwa uwajibikaji mkubwa. Pia aliahidi kuchangia mabloga ili waweze kusajili majukwaa yao kama inavyotakiwa kisheria.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Egbert Mkoko, aliwakumbusha washiriki kufuata miongozo rasmi ya uandishi wa habari za uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa blogu katika kutoa taarifa sahihi kwa jamii.
Kwa upande wake, Afisa wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Rehema Mpagama, alieleza kuwa waandishi watakaoruhusiwa kuripoti uchaguzi ni wale tu wenye ithibati, kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, aliishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa ya mafunzo hayo kupitia TCRA, akisema yatasaidia kuongeza weledi na kuimarisha usalama wa taarifa wakati wa uchaguzi.
EmoticonEmoticon