MKUU WA MKOA WA DODOMA AIPONGEZA TUME YA MADINI KATIKA MAONESHO YA NANE NANE

August 05, 2025

 



Dodoma, Agosti 5, 2025


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ametembelea Banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma na kuipongeza Tume  kwa kazi nzuri ya kuelimisha na kuhamasisha umma kuhusu fursa zilizopo katika Sekta ya Madini.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Senyamule amesema kuwa Tume ya Madini imekuwa mfano bora wa taasisi za umma zinazotekeleza majukumu yake kwa ufanisi, hususan katika kuonesha kwa vitendo namna Sekta ya Madini inavyoweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.


“Nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya. Mnaendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchimbaji, uongezaji thamani madini, na biashara ya madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa,” amesema Mhe. Senyamule.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini ikiwemo madini ya viwandani, vito, na madini ya ujenzi. Hivyo, ameitaka Tume ya Madini kuendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye sekta hiyo kwa kutumia sera na sheria zilizopo ambazo ni rafiki kwa wawekezaji.

Kwa upande wake, Maafisa wa Tume ya Madini waliopo katika banda hilo wameeleza kuwa Tume itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kushiriki katika mnyororo mzima wa shughuli za madini, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa leseni, matumizi sahihi ya teknolojia ya uongezaji thamani madini, na umuhimu wa kuuza madini kupitia masoko rasmi.



Maonesho ya Nane Nane ya mwaka 2025 yanalenga kuonesha mafanikio na fursa mbalimbali za maendeleo kutoka sekta za kilimo, mifugo, viwanda, na madini, ambapo Tume ya Madini ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki kikamilifu kuhamasisha ushiriki wa wananchi na wawekezaji katika Sekta ya Madini.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »