Na John Mapepele
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema Filamu ya Amazing Tanzania iliyowashirikisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, na mwigizaji mahiri kutoka China Bw. Jin Don imeleta mafanikio makubwa katika kipindi kifupi tangu izinduliwe nchini China mapema Mei mwaka huu.
Akizungumza kwenye mkutano na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 3, 2024 kuelezea sherehe za kufunga rasmi maadhimisho ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China, na uzinduzi wa Filamu ya Amazing Tanzania zitakazofanyika kesho jijini Dar es Salaam, Dkt. Abbasi amefafanua kuwa kumekuwa na ongezeko la takribani asilimia 69 ya watalii kutoka nchini China ukilinganisha na miaka ya nyuma.
“ Kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu kumekuwa na ongezeko la watalii kutoka 44,438 hadi takribani 54000 ambapo pia kumekuwa na ongezeko la takribani wageni 2000-3000 kwa miezi ya Juni, Julai na Septemba ukilinganisha na mwaka jana.” Amefafanua Dkt. Abbasi
Aidha, amesema mafanikio katika sekta za utalii na utamaduni yanaenda sambamba na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na jamii za kimataifa ambapo amefafanua kuwa ni kwa muktadha huo, Tanzania na China wanasheherekea miaka 60 ya Uhusiano wa Kidplomasia ulioanza tangu enzi wa waasisi wa mataifa haya yaani, Mwalimu Julius K. Nyerere wa Tanzania na Abeid A. Karume wa Zanzibar, pamoja na Mwenyekiti Mao Zedong wa China.
Ameongeza kuwa pamoja na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China katika kipindi cha miaka 60, nchi hizi zilisaini makubaliano ya kushirikiana katika sekta ya utalii tangu mwaka 2013 na kupitia makubaliano hayo, wizara imeendelea kufanya road shows nchini China, kushiriki maonesho mbalimbali ya utalii na kutangaza fursa za maeneo ya uwekezaji nchini China, ambapo pia wataalam wa sekta ya utalii wamepata mafunzo ya utalii na ukarimu nchini humo.
Ametoa rai kwa watoa huduma katika sekta ya utalii kulichangamkia soko la utalii nchini China ili kwa pamoja tushirikiane kuongeza idadi ya watalii kutoka China sambamba na mapato yatokanayo na utalii; pamoja na kuuza bidhaa za utamaduni katika soko hilo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Methusela Ntonda amesema sherehe hizo zitapambwa na wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Hazara Chana anatarajiwa kuwa mgeni rasmi ambapo viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Tanzania na China wanatarajia kushiriki.
EmoticonEmoticon