WACHAMBUZI WA SIASA NA DIPLOMASIA WATOA WITO KWA VIJANA NA WANANCHI KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMIU KWA UZALENDO NA BUSARA

October 27, 2025

 


Na Rahel Pallangyo


Wachambuzi wa masuala ya siasa, diplomasia, na maendeleo wametoa wito kwa vijana na wananchi kwa ujumla kutumia mitandao ya kijamii kwa busara na uzalendo, huku wakisisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya kina kuhusu ukweli wa taarifa wanazopokea na kusambaza, hususan katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi.


Wito huo umetolewa Oktoba 26, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa mdahalo wa 'Wajibu wa Kidijitali kwa Amani ya Nchi Kabla, Wakati na Baada ya Uchaguzi” uliofanyika katika Ukumbi wa American Corner, Makumbusho ya Taifa 

Mchambuzi wa masuala ya diplomasia na siasa, Abdulkarim Atik, amewataka vijana nchini kufanya tathmini ya kina kuhusu ukweli wa taarifa wanazopokea na kusambaza kupitia majukwaa ya kidijitali. Amesema lengo ni kuepusha taharuki na migawanyiko katika jamii inayosababishwa na habari za uwongo na propaganda zenye lengo baya.

"Ikiwa vijana watatambua ukweli wa taarifa wanazopata, itawasaidia kufanya maamuzi sahihi na kuchangia katika kulinda amani ya nchi hususan kipindi cha uchaguzi," alisisitiza Atik.

Naye Mwandishi wa habari wa Crown Televisheni, Imani Luvanga, amesisitiza kuwa mitandao ya kidijitali ni nyenzo muhimu ya mawasiliano na taarifa, na kwamba siyo mibaya kama inavyodhaniwa. Alifafanua kuwa changamoto kubwa ipo kwa watumiaji, ambao mara nyingi hueneza taarifa zisizo sahihi na zenye kuchochea migogoro.

Luvanga alieleza kuwa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii yanaweza kuleta mabadiliko chanya, yakiwemo maendeleo ya kiuchumi. Alisisitiza umuhimu wa watu kujitambua wanapotumia mitandao hiyo, kwa kuelewa sababu za kuitumia, aina ya taarifa wanazohitaji, na faida wanazotarajia kunufaika nazo.

Kwa upande wake, mdau wa siasa na maendeleo, Reeves Ngalemwa, alisisitiza umuhimu wa kuweka msingi imara wa uzalendo tangu utotoni.


"Ni muhimu kuweka mazingira ya kuwaandaa watoto kujifunza uzalendo tangu wakiwa shule za msingi ili wakue wakiwa na mapenzi ya kweli kwa nchi yao," alisema Ngalemwa.

Aliongeza kuwa lengo la kuanza kuwajenga watoto katika hatua za awali ni kuandaa kizazi chenye uelewa mpana wa masuala ya kitaifa, kinachotambua lipi ni sahihi na lipi si sahihi, hususan katika zama hizi za kidijitali. Ngalemwa alihitimisha kwa kusema kuwa msingi huu imara utasaidia kujenga Taifa lenye vijana wanaopenda na kulinda maslahi ya nchi yao.

Mchambuzi wa masuala ya vyombo vya habari na mpiga picha maarufu, Isa Michuzi, amesisitiza kwamba wananchi wanatakiwa kujua na kuyachunguza kwa kina mambo mengi yaliyomo katiukja mitandao kwani mengine ni propaganda za chuki.

"Watu wanastahili kuangalia kwa umakini sana. Propaganda inaweza kuwa nzuri au mbaya. Tumefika hapa si kwa bahati mbaya, ni matokeo ya kuruka hatua. Kila mtu awe mlinzi wa taifa," alieleza Michuzi.


Alionya kuwa kutokuwa na uangalifu katika kusambaza taarifa hufanya jamii iingie katika migogoro isiyo ya lazima.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TBN , Beda Msimbe alizungumzia haja ya vijana wa sasa kuwa na ndoto zilizojengwa imara katika muktadha wa kitaifa na uzalendo huku wakiangalia mambo katika upana wake na si kuchukua tukio moja tu.


Alisema vijana wanahitaji msingi  imara ili maamuzi yao yawe ya kusonga mbele badala ya kuumiza taifa. Lengo ni kuweka maslahi ya Taifa mbele katika matumizi yao ya mitandao ya kijamii na katika kufanya maamuzi ya kisiasa.


Mdahalo huo uliokuwa chini ya Mwenyekiti Jukwaa la Wachambuzi, Magid Mjengwa ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wahariri wa mawasiliano ya kidijitali, wanabloga kutoka Taasisi ya Tanzania Bloggers Network (TBN), wanafunzi wa Chuo cha Diplomasia, wadau wa amani, na waandishi wa habari.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »