-Wananchi waipokea kwa kishindo
-Klabu za Nishati Safi ya Kupikia zaanzishwa mashuleni
-Walimu na Wanafunzi waipongeza REA waahidi kuwa mabalozi
-Lengo ifikapo 2034; 80% ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia katika kila kona ya Nchi ili kuhakikisha ustawi wa wananchi kupitia matumizi endelevu na salama ya nishati safi ya kupikia.
Hayo yameelezwa na Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Daniel Mwandupe wakati wa kampeni ya uelimishaji na uhamasishaji wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia katika Shule ya Sekondari Mbawala Wilayani Mtwara Mkoa wa Mtwara.
“Leo hii tumefika hapa kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuleta mabadiliko ya fikra na tabia katika jamii kwa ujumla; REA imedhamiria kuona wananchi wanaongeza uelewa wa faida zinazopatikana kwa kutumia nishati safi,” alifafanua Mha. Mwandupe.
Mha. Mwandupe alitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni ya nishati safi ya kupikia hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta hiyo.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka REA, Jaina Msuya alisema dhamira ya kuanzisha Klabu ya Nishati Safi ya Kupikia shuleni hapo ni kuongeza hamasa kwa wanafunzi ili waweze kutambua umuhimu wake sambamba na kuongeza ushiriki wao katika kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Leo hii tumezindua rasmi Klabu ya Nishati Safi ya Kupikia hapa shuleni na tumetoa zawadi ya jiko banifu kwa Klabu na pia tumejadili masuala mbalimbali na tumeona namna ambavyo wanafunzi wamehamasika na hii ni dalili njema kwamba tutafanikiwa kwa kishindo kufikisha lengo la Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia,” alisisitiza Jaina.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mbawala, Amina Mtuvenge aliishukuru na kupongeza REA kwa kufika shuleni hapo kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo.
“Tumeelezwa uwepo wa mpango maalum unaoandaliwa na REA wa uwezeshwaji kwa taasisi zinazoandaa chakula na kulisha zaidi ya watu 100 kwa siku kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, taarifa hii tumeipokea vyema na tumehamasika kuchangamkia fursa hii mapema iwezekanavyo ili tubadilishe aina ya nishati tunayotumia kupikia hapa shuleni,” alisisitiza Mwalimu Mtuvenge.
Aidha, kwa nyakati tofauti wanafunzi waliipongeza REA kwa ubunifu inaoufanya na waliahidi kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia majumbani mwao na kwa jamii zinazowazunguka.








EmoticonEmoticon