WAZIRI MAVUNDE AAGIZA MAAFISA MADINI WAKAZI WA MIKOA KUTUMIA MAGARI 25 YALIYOZINDULIWA

October 21, 2024




WAZIRI wa Madini Mhe Anthony Peter Mavunde ametoa Rai kwa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini kuhakikisha kuwa Magari 25 yaliyozinduliwa leo yanakwenda kufanya kazi iliyokusuduwa ambayo ni majukumu yaliyopo ndani ya Wizara ya Madini na si vinevyo.

Na kuongeza kuwa, pia hategemei kuwa magari hayo yatakwenda kukaa badala ya kufanya vitu vyenye manufaa kwa Wizara hiyo.

Mhe Mavunde amesema hayo mapema leo hii Oktoba 21,2024 Jijini Dodoma wakati akizindua magari Mapya 25 kwaajili ya kusambaza kwenye Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini.

"Rai yangu mpo hapa Watumishi wa Serikali, Magari haya yakatumike kwa kazi iliyokusudiwa na tunayafunga magari haya yoye GPS ili tuwe na uwezo wa kuyaona tukiwa makao makuu na kazi ambayo yatakuwa yanafanya katika nyakati zote".

"Lakini pia hatutegemei magari kwenda kukaa wala kufanya shughuli ambazo sio za msingi za Wizara ya Madini. Kwahiyo hili pia naamini Katibu Mkuu mmezingatia maelekezo yangu tangu awali kuwa magari hayo yoye yafungwe GPS".

Aidha Mhe. Waziri Mavunde amesema kuwa Wizara imepanga kununua magari 89 na pikipiki 140 kama sehemu ya uboreshaji wa usimamizi wa Sekta ya Madini kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa hasa kwenye usimamizi wa ukusanyaji wa maduhuli na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato na utoroshaji wa maduhuli.

Amesema kuwa, magari yaliyozinduliwa 25 ni awamu ya kwanza ya magari 89 yanayotarajiwa kuletwa sambamba na pikipiki 140 zitakazosambazwa kwenye ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa zilizopo nchi nzima.

Pamoja na yote hayo Mhe. Mavunde ametumia fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele Sekta ya Madini kwa kuiongezea bajeti Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 mwaka 2023/2024 hadi shilingi bilioni 231 katika mwaka wa fedha 2024/2025

“ Ongezeko hili ni dhahiri kabisa Dkt. Samia anatamani kuona Sekta ya Madini inaendelea kuimarika na mchango wake kuongezeka kwenye Pato la Taifa hasa kwenye ukusanyaji wa maduhuli, mathalan katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 tumepewa lengo la kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni Moja ambapo ndani ya siku 90 tumeweza kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 287 ikiwa ni asilimia 106 ya lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 249 ndani ya kipindi husika".

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde ameelekeza magari yote kufungwa GPS kwa ajili ya kuangalia mwenendo wake ili kuhakikisha yanatumika katika matumizi yaliyokusudiwa.

“Magari yote yatafungwa GPS ambapo Makao Makuu tutakuwa na uwezo wa kuona mwenendo wa magari kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hasa kwenye shughuli za ukusanyaji wa maduhuli na ukaguzi wa migodi ya madini".

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amempongeza Waziri Mavunde kwa jitihada zake za usimamizi wa Sekta ya Madini na kuwataka watendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha wanaonesha matokeo chanya kwenye utendaji kazi wao.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo pamoja na kuishukuru Wizara ya Madini kwa magari husika lakini ppia amesema magari haya yatatumika kama chachu ya Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwenye ongezeko la makusanyo ya maduhuli.

Haya ni magari 25 kati ya 89 yanayohotajika na magari yote 89 yatakayonunuliwa yatagharimu zaidi ya shilingi bilioni 18.





Share this

Related Posts

Previous
Next Post »