SHIRIKA AMEND,JESHI LA POLISI TANGA WAENDELEA KUTOA ELIMU YA USALAMA BARABARANI

April 17, 2024

 


Ofisa Miradi kutoka Amend Tanzania Scholastica Mbilinyi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoa elimu kwa Madereva wa Pikipiki maarufu kama Bodaboda,Bajaji na Madereva wa Daladala katika Stendi ya Pongwe Jijini Tanga
Ofisa Miradi kutoka Amend Tanzania Scholastica Mbilinyi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoa elimu kwa Madereva wa Pikipiki maarufu kama Bodaboda,Bajaji na Madereva wa Daladala katika Stendi ya Pongwe Jijini Tanga
Mkuu wa Usalama Barabarani,kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga Mrakibu wa Polisi Wiliam Mwamasika
Mkuu wa Usalama Barabarani,kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga Mrakibu wa Polisi Wiliam Mwamasika akizungumza na madereva wa bodaboda pikipiki maarufu kama bodaboda,bajaji na daladala






Na Oscar Assenga,TANGA


Shirika la Amend Tanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Switzerland Nchini,wameendesha zoezi la utoaji wa Elimu ya Usalama Barabarani kwa Madereva Daladala na Bodaboda Jiji la Tanga ikiwa ni sehemu ya kupunguza na kutokomeza ajali za barabarani zinazotokana na uzembe wa madereva.

Akizungumza wakati wa utoaji wa Elimu hiyo ya Usalama Barabarani iliyofanyika Aprili 16,2024 katika Stendi ya Pongwe Jijini hapa,Ofisa Miradi kutoka Amend Tanzania Scholastica Mbilinyi, amewaambia waandishi wa habari kuwa lengo ni kuwafikia Madereva 500 na mpaka sasa Madereva 300 tayari wameshafikiwa katika awamu ya kwanza,

Alisema kwamba wamewafikia madereva wa pikipiki maarufu kama (Bodaboda) kuwapa mafunzo ya Usalama Barabarani na waliohitimu wamepewa vyeti huku akieleza wataendelea na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa awamu ya pili ambao utaanza mwezi mei mwaka huu na itakuwa endelevu.

Scholastica aliwataka Madereva wa vyombo vyote vya moto kuzingatia sheria za Usalama Barabarani ili kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na uzembe wa Madereva,

"Niwaombe Madereva wote hususani wa Bodaboda tuzingatie Usalama Barabarani tusibebe watoto chini ya miaka 9 kwa sababu hawana uwezo wa kuhimili mikikimikiki ya Barabarani na maisha yako ni muhimu zaidi kuliko pesa wanayoitafuta"Alisema


" Tuzingatie Usalama kwanza ili ajali zipungue zibakie zile ambazo haziepukiki ikiwemo kupasuka kwa tairi ,kukatika kwa stelingi au tatizo lolote la kiufundi katika vyombo vyetu vya moto"Alisisitiza Scholastica

Kwa upande wake Mkuu wa Usalama Barabarani,kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga Mrakibu wa Polisi Wiliam Mwamasika aliwataka madereva wote kwenda darasani kama sheria inavyowataka kufanya hivyo,


"Tupo hapa kutekeleza wajibu tuliopewa na Serikali ambayo ni nyie wananchi lakini sote tunafahamu kuwa Serikali mwaka jana ilitoa maelekezo ya madereva wote kwenda kusoma pamoja na kuhakiki leseni zenu,wapo baadhi yenu wametekeleza maagizo ya Serikali"Alisema


Hata hivyo alisisitiza umuhimu wao kuhakikisha wanalitekeleza suala la kusoma huku akiwataka wasifanye jambo kwa shuruti kwa sababu elimu wanayoenda kuipata kwa ajili ya manufaa yao hivyo hawana haja yakulazimishana.

Aidha aliwaonya Madereva wa Daladala kuacha tabia ya kusimamisha Daladala zao kwa muda mrefu kwenye maeneo yasiyokuwa na vituo katikati ya Jiji hili lenye mpangilio mzuri wa namba za Barabara za mitaa,

"Kwa Bahati mbaya wakati wanapangilia Jiji hili walisahau kuweka vituo vingi vya Daladala, hivyo sisi tumeona ni busara tu kwa baadhi ya maeneo kwenye Barabara za namba Daladala inaweza ikasimama kwa muda mfupi sana ili kuepusha msongamano unaoweza kujitokeza,unatakiwa utumie muda mfupi sana kupakia au kushusha abiria wako kwenye vituo tulivyoviruhusu" Alisisitiza SP.Mwamasika

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »