Na OR – TAMISEMI, Arusha
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Elimu nchini ili kuhakikisha changamoto zinazoikabili Sekta ya elimu zinatatuliwa kwa kufanya maboresho mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 24 Juni, 2025 Jijini Arusha katika ukumbi wa Kibo Palace Hotel na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu na Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt Emmanuel Shindika kwa niaba ya Bw. Atupele Mwambene, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo alisema ili kuhakikisha Sekta hiyo inakwenda vizuri, Serikali itawashirikisha Wadau wote wa Elimu waliopo ndani na nje ya nchi, wa kitaifa na kimataifa kuendelea kuzikabili changamoto za Sekta hiyo hapa nchini kama vile ajira za walimu na ujenzi wa miundombinu.
Aidha, Dkt. Shindika alisema Serikali inafuatilia kwa karibu na kufanya utafiti kwa kutumia taarifa za kimfumo za kujua maeneo yaliyo na uhaba wa walimu na pindi wanapoajiriwa walimu wapya basi hupelekwa kwenye maeneo yenye upungufu wa walimu hususani maeneo ya pembezoni yenye uhaba mkubwa wa walimu.

“Ofisi ya Rais TAMISEMI imejipanga vema katika kupanga walimu kulingana na mahitaji ya eneo husika na hivyo, hakutaweza kutokea mlundikano wa walimu wengi sehemu moja kwani kabla ya kuwapanga, tayari Wizara inajua wapi kuna mahitaji kutokana na utafiti ambao utakuwa umefanywa” alisisitiza Dkt. Shindika.
Naye Bi. Stella Mayenje Msimamizi wa Miradi ya Ufadhili wa Serikali ya Sweden kwa Serikali ya Tanzania alisema wamekutana kama Wadau wa Elimu Tanzania kufanya tathmini ya pamoja kama ambavyo walikubaliana na Serikali na Wadau wote mwaka 2022 (Midterm Review Partnership Compact, 2025) lakini pia kama wadau, wamejikita katika kusaidia ufadhili hususani Sekta ya elimu kwa kuangalia wapi wanafanya vizuri na wapi kunahitaji maboresho kwa mfano kuimarisha mipango ya kuwa na walimu wa kutosha, mazingira ya kufundishia na kujifunzia na masuala ya jinsia.

Bi. Mayenje aliongeza kuwa katika Mradi wa GPE LANES II ulifanikiwa kwa asilimia 95.4 na katika Mradi wa sasa wa Kuboresha Kada ya Ualimu (GPE TSP), umekuja na vigezo vya kuangalia takwimu za walimu wanaoajiriwa kama ipo sawa na wanafunzi waliopo shuleni na hapa alisema kama sehemu ya motisha kwa Serikali upande wa ufadhili unatoa Dola za Kimarekani 10,000 kwa kila walimu 3,000 walioajiriwa na Serikali ambapo fedha hizo za Msaada hupelekwa kufanya maboresho kwenye masuala ya elimu yaliyoainishwa.
Kwa upande wake Dkt. Jordan Busingu Mshauri wa Elimu kutoka Ubalozi wa Uingereza, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Wadau wa Maendeleo, alisema kikao kazi hicho cha mapitio kina lengo kubwa kwao kama kama Wadau wanaoshirikiana na Serikali katika kuhakikisha elimu inamfikia kila mtoto na hakuna anayeachwa nyuma kama vile kuweka usawa (equity) katika utoaji wa elimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kufanya tathmini yao na Serikali kuhusu maendeleo ya Sekta ya elimu nchini.

Kikao Kazi cha siku mbili kwa mwaka 2025 kinaangazia kufanya mapitio ya Kati ya Mpango wa Ushirikiano wa Wadau mbalimbali wa elimu kutoka ndani na nje pamoja na Wadau wa Maendeleo ili kutathmini maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini kwa kuibua hoja za nini kifanyike katika kuendeleza na kukabiliana na changamoto za elimu.
EmoticonEmoticon