📌Shilingi bilioni 35 kupeleka nishati safi magereza yote nchini
📌Mitungi ya gesi 653 kupatiwa watumishi magereza Tanga
📌Mha. Saidy asisitiza uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi wa magereza na wananchi ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024 – 2034).
Hayo yamebainishwa leo Juni 24, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu wakati wa uzinduzi wa kugawa majiko ya gesi kwa watumishi wa magereza iliyofanyika Gereza Kuu la Maweni jijini Tanga.
"Hii yote ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 zihame kutoka katika matumizi ya nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia, " Ameongeza.
Vile vile ameongeza kuwa, Magereza yote ya mkoa wa Tanga tayari yanatumia makaa ya mawe ya Rafiki Briquette unaozalishwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mha. Hassan Saidy amewataka watumishi wa magereza kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu matumizi na umuhimu wa nishati safi ya kupikia ili kuifanya nishati hiyo kuwa endelevu, pia ni chachu kwa wananchi katika kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa.
Amesema kuwa, gharama ya mradi wote ni zaidi ya shilingi Bilioni 35.2 ambapo Wakala wa Nishati Vijijini unatoa ruzuku ya shiling bilioni 26.5 Sawa na asilimia 75.4 ya gharama ili kuwezesha utekelezaji wake.
Kwa upande wake, ACP Nade Baynit, Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga ameishukuru REA kwa kuwezesha watumishi magereza kutumia nishati safi ya kupikia. Aidha, amewakata watumishi hao kuchangamkia fursa hiyo inayotolewa na REA kwa watumishi wa magereza kwa kujipatia mtungi wa gesi na majiko ya gesi ya sahani mbili bure na waeendelee kuwa mabalozi wa nishati hiyo kwa wananchi.
Naye, Mratibu wa nishati safi kutoka kampuni ya Lake Gas Ltd Bw. Ramadhani Siasa amesema watatekeleza mradi huo kwa kuzingatia makubaliano ya Mkataba wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia pamoja na kutoa elimu, kuhamasisha wananchi ili kuchochea matumizi ya nishati hiyo.
![]() |
![]() |
EmoticonEmoticon