KANISA LA ANGLIKANA DAYOSISI YA DAR YAANDAA BONANZA KUCHANGIA UJENZI WA JENGO LA KITEGA UCHUMI

June 28, 2025
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam kupitia Mtaa wa Mtakatifu Andrea Magomeni, limeandaa Bonanza maalum la kuwakutanisha waumini wake kwa ajili ya kufanya mazoezi ya pamoja, likiwa ni lengo la kuimarisha afya ya kimwili na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

Bonanza hilo pia limebeba ujumbe wa Neno kutoka  Hagai 1: 8 na kupewa Kauli Mbiu ya TUMEAMUA kuelekea kwenye kilele cha harambee kubwa ya ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Kanisa la Mtakatifu Andrew Magomeni, inayotarajiwa kufanyika tarehe 06 Julai, 2025.

Akizungumza katika viwanja vya Magomeni Kota wakati wa uzinduzi wa Bonanza hilo, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Mhashamu Jackson Sosthenes Jackson, amesisitiza umuhimu wa mazoezi kwa mwili wa binadamu kama sehemu ya huduma ya kiroho.

"Mwili wenye afya ni sehemu ya mwili wa Kristo. Tunapojali miili yetu, tunalitumikia pia Kanisa," amesema Askofu Sosthenes.

Ameongeza kuwa bonanza hilo ni sehemu ya dhamira pana ya kujenga jengo la kitega uchumi la Kanisa la Mtakatifu Andrew Magomeni, ikiwa ni sehemu ya kujiimarisha kiuchumi na kuendeleza kazi za kiroho na kijamii.

Katika hatua ya kutia moyo, Askofu amepongeza waumini kwa kujitolea kwao hadi kufanikisha ukusanyaji wa zaidi ya asilimia 70 ya lengo la Shilingi milioni 60 zinazohitajika kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa jengo hilo la kitega uchumi.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya moyo wa kujitoa na mshikamano miongoni mwa waumini.

Askofu Sosthenes ametumia fursa hiyo kuzihimiza makanisa mengine nchini kuiga mfano huo kwa kuanzisha shughuli za kuimarisha afya za waumini pamoja na kuchangia maendeleo ya kanisa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »