Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kifedha baada ya amana zake kuongezeka na kufikia shilingi trilioni 1.3, hatua inayotokana na mafanikio ya utoaji mikopo katika mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Januari 29, 2026, Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Fedha wa benki hiyo, Kaanael Nnko, amesema mwaka uliopita benki ilikuwa na amana za shilingi bilioni 900, lakini hadi kufikia Desemba 31, 2025, ziliongezeka hadi trilioni 1.3 sawa na ukuaji wa asilimia 44.
“Mwaka jana tulipokuwa tunaongea tulikuwa na amana za bilioni 900, lakini tulipofunga Desemba 31 tumefikia trilioni 1.3. Huu ni ukuaji wa asilimia 44,” amesema Nnko.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanaenda sambamba na benki hiyo kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Kwa upande wa faida, Nnko amesema TADB ilipata faida ya shilingi bilioni 24.6 mwaka uliopita, huku mwaka unaoishia Desemba 2025 faida ikiongezeka hadi shilingi bilioni 35.3, sawa na ukuaji wa asilimia 43.
“Tulifanikiwa kukuza mapato na kudhibiti gharama za uendeshaji wa benki, hivyo kupata faida kubwa zaidi,” ameeleza.
Kuhusu mikopo chechefu, alisema imepungua na kufikia asilimia 2.5, kiwango ambacho kiko chini ya ukomo wa asilimia tano uliowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“BoT imetaka mikopo chechefu isivuke asilimia tano. Sisi tumefunga tukiwa na asilimia 2.5, maana yake mikopo yetu inafanya vizuri,” amesema.
Kwa mwaka huu, Nnko amesema benki inatarajia kutoa mikopo ya shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo na mnyororo mzima wa thamani, kuanzia kwa wakulima wadogo hadi wakubwa.
Ameongeza kuwa TADB inashirikiana na benki 19 za biashara katika utoaji wa mikopo kwa wakulima na wafugaji nchini, hatua inayochochea maendeleo ya kilimo na ujasiriamali vijijini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa TADB, Afia Msigge, amesema benki imekuwa ikitoa mikopo ya moja kwa moja kwa wakulima, pamoja na kutoa dhamana kwa wakulima wadogo kupitia ushirikiano na benki za biashara.
Amesema mwaka jana TADB ilitoa mikopo kwa ongezeko la asilimia 67 ikilinganishwa na mwaka 2024, ambapo jumla ya shilingi bilioni 429 zilitolewa na kunufaisha wakulima 233,434 kote nchini.
Msigge ameongeza kuwa benki ilitoa mikopo katika miradi 98 ya uzalishaji, miradi 72 ya uchakataji wa mazao, pamoja na ujenzi wa maghala 44 ya kuhifadhi mazao baada ya mavuno.
Aidha, amesema TADB imekuwa ikipeleka elimu ya masoko kwa wakulima wadogo na kuwaunganisha na masoko mbalimbali ili kuhakikisha wanauza mazao yao kwa wakati na kwa tija.
EmoticonEmoticon