NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
WAAJIRI wamesema pesa
wanayochangia kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) haipotei bure kwani
ni kwa maslahi ya pande tatu, Mwajiri, Mfanyakazi na Serikali.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
yaliyofikia kilele leo Julai 13, 2023 wameishukuru Serikali kwa kuanzisha Mfuko
wa Fidia kwa Wafanyakazi kwani unatoa hakikisho la usalama wa Mfanyakazi.
“Tayari tumeanza
kuchangia, tuchukue nafasi ya kuelimishana ndani kwamba iko fursa ndani ya WCF
kuwahudumia wafanyakazi pindi wanapokumbwa na madhila wawapo kazini.” Alisema
Akbarali ambaye ni mwajiri kutoka kampuni yakutengeneza magari makubwa ya GF
iliyoko Kibaha.
Kiwanda cha GF kina
miaka mitatu tangu kianze kufanya kazi na kina jumla ya wafanyakazi zaidi ya
300 ambao wanachangiwa kwenye Mfuko wa WCF.
Bw. Akbarali alisema,
alifika kwenye banda la WCF ili aweze kupata uelewa zaidi kuhusu huduma
zitolewazo na WCF ingawa kampuni yake tayari ilijisajili kama takwa la
kisheria.
Naye Mkurugenzi wa
Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ambaye naye ni mwajiri Bw. Elihuruma
Mabelya amesema Manispaa ya Temeke inao wafanyakazi zaidi ya 5,600 lakini pia
ina idadi kubwa ya viwanda vikiwemo vikubwa na vidogo hali inayofanya WCF kuwa
mdau muhimu wa Manispaa hiyo.
“WCF kwetu kama Temeke
imekuwa kama mkombozi, kwasababu wafanyakazi wanapopatwa na ajali au matatizo
wakati wa utekelezaji wa majukumu yao Mfuko unakuja kusaidia na hivyo
kutoathiri uzalishaji mali unaoendelea ndani ya Wilaya yetu,” alisema.
Aliipongeza WCF
kutokana na kuchukua jukumu la kumuinua mwananchi ambaye ni Mfanyakazi na
mwsiho wa siku kuinua uchumi wa Halmashauri na kuinua uchumi wa Taifa.
Naye Bw. Dofrian Junwalji
kutoka Taasisi ya Trias Tanzania inayowawezesha Wajasiriamali alisema elimu
aliyoipata kwenye banda la WCF imemuwezesha kupata uelewa zaidi na ametambua
umuhimu wa WCF kiuchumi kwa mwajiri na mwajiriwa.
“Mfanyakazi anapoumia maana yake atakuwa hazalishi, kwahivyo WCF ina beba jukumu la kumuwezesha kujikimu kimaisha kwa kumlipa fidia kwa hivyo mzunguko wa fedha unakuwepo, ataendelea kupata mahitaji yake kama vile chakula, kulipia pango na mahitaji mengine.” Alifafanua Bw. Junwalji.
Alitaja manufaa mengine
kuwa ni pale Mwajiriwa anapokumbwa na matatizo ya kuumia au kuugua WCF
inamuhudumia na hivyo mwajiri anabaki akiendelea na shughuli zake za uzalishaji
na ikibidi Mfuko unamfidia gharama alizoinhia mwajiri kumuhudumia manyakazi
wake.
‘Ningependa kuwashauri
waajiri kujisajili na Mfuko kwani
kwakufanya hivyo matokeo ya uamuzi wa kufanya hivyo yatakuja kuonekaan
baadaye na uchangiaji wenyewe ni asilimia 0.5 tu ya mshahara wa mwajiriwa.”
Alihitimisha.
Akitoa tathmini yake
mara baada ya kutemebela banda la WCF na kujionea jinsi waajiri na wafanyakazi
wanavyopatiwa huduma, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi alisema, WCF inafanya kazi nzuri
licha ya kuwa na muda mfupi tangu kuanzishwa kwake.
“Nampongeza sana
Mkurugenzi Mkuu Dkt. Mduma pamoja na Bodi ya Wadhamini, wanafanya kazi kubwa na
nzuri na ya mfano kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.” Alisema.
Katika eneo la utoaji
huduma, alisema zaidi ya asilimia 80 ya huduma zote za WCF zinatolewa kwa njia
ya TEHAMA.
“WCF ina watu wenye
weledi wa kutosha lakini niwahakikishie waajiri na wafanyakazi kuwa
ustahimilivu wa Mfuko huu ni wa uhakika hata kama itatokea 2050 Mfuko
haujafanya chochote unao uwezo wa kuwahudumia wateja wake.” Alitoa hakikisho.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amewahakikishia waajiri na wafanyakazi
kuwa Mfuko uko imara katika kuhakikisha unatekeleza wajibu wake wa kulipa fidia
stahiki na kwa wakati endapo mfanyaklazi ataumia, kuugua au kufariki kutokana
na kazi.
“Tunayafanya haya ili
kuhakikisha kwamba wawekezaji waliopo sasa na wanaokuja wakute nguvu kazi ya
Tanzania ikiwa salama, na wale watakaopatwa na madhara yatokanayo na kazi Mfuko
wa WCF utatumika kuwalipa fidia zao stahiki, kuwalipia matibabu yao ili
kuhakikisha wanarejea kazini haraka iwezekanavyo.” Alitoa hakikisho.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila (mwenye balaghashia) akishukuru baada ya yeye na ujumbe wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Mobhare Matinyi (wapili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Temeke Bw. Elihuruma Mabelya, walipopewa elimu kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge (kulia).
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar (kulia) akifafanua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na WCF kwa baadhi ya waajiri hawa waliotembelea banda la Mfuko huo.
EmoticonEmoticon