Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina (kulia) akiangalia mashine ya kukamulia maziwa mara baada ya kufika kwenye banda la Kampuni ya pembejeo za Mifugo ya "Afrifarm" leo (26.10.2022) ikiwa ni muda mfupi kabla ya kufungua kongamano la Chama cha Wanataaluma wa sayansi ya Uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) linalofanyika jijini Arusha
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina (kushoto) akielezea umuhimu wa hereni za kielektroniki alipofika kwenye banda la Kampuni ya pembejeo za Mifugo ya "Afrifarm" muda mfupi kabla ya kufungua kongamano la Chama cha Wanataaluma wa sayansi ya Uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) leo (26.10.2022) jijini Arusha. Kulia ni Afisa Mauzo wa kampuni hiyo Bw. Emanuel Senge.Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Charles Mhina (wa kwanza kushoto) na baadhi ya viongozi wa Chama cha Wanataaluma wa sayansi ya Uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) wakifuatilia uwasilishwaji wa maandiko ya wanataaluma mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kongamano la chama hicho linalofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 26-28, 2022
Dkt. Kizima abainisha namna TSAP inavyo wainua wataalam mbalimbali wa sekta za Mifugo na Uvuvi
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza zoezi la utekelezaji wa mpango wa mabadiliko wa miaka 5 wa Sekta ya Mifugo ambao unatarajia kutumia zaidi ya shilingi Trilioni 2 mpaka kukamilika kwake.
Hayo yamesemwa leo (26.10.2022) na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kwa upande wa Sekta ya Mifugo Dkt. Charles Mhina katika hotuba yake ya Ufunguzi wa kongamano la Chama cha wanataaluma wa sayansi ya uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) uliofanyika kwenye Ukumbi wa “Olasit Garden” jijini Arusha.
Dkt. Mhina ametumia jukwaa hilo kuwasisitiza wataalam waliopo kwenye chama hicho kuendelea kufanya tafiti zenye tija na zinazolenga kuboresha ufugaji na maisha ya wafugaji kwa ujumla ili kuirahisishia Serikali katika utekelezaji wa Mpango huo.
“Mpango huu unalenga kuboresha sekta ya Mifugo kwa ujumla kuanzia katika eneo la uzalishaji wa mifugo hasa katika eneo la uhimilishaji na matumizi ya madume bora ya mbegu, uzalishaji wa malisho kupitia mashamba darasa ambayo tunaenda kuyaanzisha kwenye Halmashauri takribani 100 ili wafugaji wetu waweze kujifunza namna ya kulima mbegu na malisho yenyewe kuanzia kupanda hadi kuyavuna na lengo letu ni kuhakikisha mbegu hizo zinapatikana kwenye maduka mbalimbali ya pembejeo hivyo ninaamini kupitia maandiko yenu kama wanataaluma tutaendelea kupata suluhu ya namna ya kufanikisha hayo ” Amesisitiza Dkt. Mhina.
Dkt. Mhina ameongeza kuwa eneo jingine ambalo Mpango huo utaliangazia ni lile la afya ya Mifugo ambapo Wizara yake imeendelea kuongeza dawa za kuogeshea mifugo na chanjo za magonjwa mbalimbali yanayoikabili mifugo hapa nchini.
“Lakini pia kupitia mpango huo tunaendelea kuboresha huduma za ugani, tafiti na uanagenzi ambapo tumeanzisha Vituo atamizi 8 vinavyolenga kuwasaidia vijana waliopo mtaani wenye taaluma ya ufugaji kujifunza kwa vitendo namna ya kufanya unenepeshaji wa Mifugo ambapo tunawapatia mifugo ya kunenepesha, tunawafundisha namna ya kunenepesha na wakimaliza mafunzo tunawagawia ng’ombe hao kama mtaji wa kuanzia huko waendako na kwa mwaka huu tumeanza na vijana 240” Amebainisha Dkt. Mhina.
Katika hatua nyingine Dkt. Mhina amewapongeza wataalam wanaounda Chama cha wanataaluma wa sayansi ya uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) kwa kuandaa maandiko ya tafiti zao na kuziwasilisha ili zijadiliwe kabla ya kuchapishwa kwa matumizi ya sekta ya Ufugaji ambapo amebainisha kuwa utekelezaji wake utakuwa na tija kwa mfugaji mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt. Jonas Kizima amesema kuwa lengo la kufanyika kwa kongamano hilo kila mwaka ni kujadili na kuchambua mada za kisayansi zinazoonesha matokeo ya utafiti ili matokeo hayo yapelekwe kwa wadau mbalimbali wa sekta za mifugo na Uvuvi.
“Uchambuzi wa mada hizo ukishakamilika utatupa picha ya aina ya teknolojia zinazopaswa kutumika ili kuongeza tija katika sekta za Mifugo na Uvuvi na matokeo hayo tutayaweka kwenye chapisho kwa ajili ya kutumiwa na wadau wa sekta hizo” Ameongeza Dkt. Kizima.
Dkt. Kizima amesema kuwa machapisho yote ya kisayansi yanayopitishwa kupitia kongamano hilo la wataalam huwekwa kwenye majarida ya kisayansi yanayopatikana mitandaoni ambayo pia huweza kumsaidia mtaaluma husika kupanda cheo kwenye ajira yake na kumruhusu kuyawasilisha katika majukwaa mbalimbali ya wanataaluma.
Kongamano hilo la 49 la wanataaluma litafanyika kwa muda wa siku 3 kuanzia Oktoba 26-28 ambapo mwaka huu linaambatana na dhima isemayo “kuenzi matokeo ya teknolojia na ubunifu ili kuongeza chachu katika maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi.
EmoticonEmoticon