WALENGWA WA TASAF WILAYANI CHATO MKOANI GEITA WACHANGAMKIA HUDUMA ZA MFUKO WA BIMA YA AFYA YA JAMII

March 10, 2018

Takribani kiasi cha Shilingi Milioni 140 zimepatikana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita baada ya Wananchi wanaopata huduma za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- katika Wilaya ya Chato Mkoani Geita kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii-CHF.

Mkuu wa Wilaya ya Chato Bw.Shaaban Ntarambe amewambia Wandishi wa Habari wanaotembelea Mkoani Geita kuona namna Wananchi wanaonufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanaovyotumia fursa hiyo kuwa pamoja na kuanzisha shughuli za kiuchumi ,walengwa hao pia wamehamasishwa kujiunga na CHF kwa kuchangia kiasi cha shilingi 10,000 kwa mwaka na kupata huduma za matibabu kwa kipindi chote cha mwaka.

Amesema kumekuwa na mwitikio mzuri kwa Walengwa hao wa TASAF kujiunga na huduma za CHF kwa kutumia sehemu ya ruzuku wanayoipata kupitia utaratibu wa uhawilishaji fedha na hivyo kuboresha afya zao na kupunguzia mzigo wa serikali kuwahudumia hususani pale wanapohitaji huduma ya matibabu.

Kwa Upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chato Dr Athanus Ngambakubi amesema katika vijiji ambavyo TASAF inatoa huduma kwa Kaya Maskini ambazo zimejiunga na CHF,Wataalam wa Afya hawalazimiki kutumia nguvu kubwa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kupata huduma za matibabu hospitalini kinyume na ilivyokuwa kabla ya kuanza kwa Mpango huo.

“Tunaishauri Serikali kupitia TASAF kusambaza huduma za Mpango huo katika vijiji vyote ili wananchi waweze kunufaika nayo kwa pamoja” amesisitiza Dr Ngambakubi .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chato Bw,Bathlomeo Manunga amesema tangu kuanza kwa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halamshauri hiyo kumekuwa na mabadiliko chanya hususani kwa kaya zilizokuwa zinaishi katika hali ya umaskini mkubwa wa kipato.

Amesema Walengwa wengi kwa sasa wameanza kujiwekea rasilimali hususani mifugo wakiwemo mbuzi,ng’ombe na kuku huku wengine wakiboresha makazi yao kwa kutumia sehemu ya mapato kupitia utaratibu wa Uhawilishaji fedha unaotekelezwa na TASAF.

Naye Afisa Elimu wa Wilaya ya Chato, Bw. Angaselina Kweka amesema tangu kuanza kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo ,kumekuwa na ongezeko la mahudhurio ya wanafunzi wanaotoka kwenye kaya za Walengwa kutoka wastani wa asilimia 79 mwaka 2015 hadi asilimia 91 mwaka 2018.

Amesema ongezeko hilo limetokana na hali ya ulinganifu wa haiba kwa wanafunzi ambao kabla ya kuanza kwa shughuli za Mpango walishindwa kuhudhuria masomo kwa kukosa sare za shule,viatu,madaftari na hata lishe mambo ambayo kwa sasa yamepatiwa ufumbuzi kwani suala la mahudhurio ya wanafunzi wanaotoka kwenye kaya za Walengwa ni mojawapo ya masharti ya kuendelea kupata ruzuku inayotolewa kupitia TASAF.

“ Kwa sasa huwezi kutofautisha mtoto anayetoka katika kaya maskini na ile yenye kipato wawapo darasani kwani wote wanakuwa nadhifu hali inayoleta usikivu kwao na kufanya vizuri katika masomo yao ” Amesisitiza Afisa Elimu huyo.

Afisa elimu huyo pia amesema Wazazi wa watoto wanaotoka kwenye kaya za walengwa wanalazimika kwenda shuleni kufuatilia mahudhurio ya watoto wao ili kuepuka kukatwa ruzuku pale inapobainika kuwa mahudhurio ya watoto wao ni hafifu jambo lililosaidia kuboresha taaluma katika wilaya hiyo ambayo ni miongoni mwa wilaya 10 bora kitaifa katika kufaulisha wanafunzi.
Mmoja wa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF ,Esther Seleman mkazi wa kijiji cha Mabalasana katika halmashauri ya wilaya ya Geita akiwaonyesha Waandishi wa Habari (hawapo pichani) shamba la Mpunga ambalo amelima kwa kutumia sehemu ya ruzuku aliyoipata kupitia utaratibu wa uhawilishaji fedha kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato.
Mmoja wa Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Isamilo katika halmashauri ya wilaya ya Geita akiwa katika shughuli ya kushona nguo kwa kutumia cherahani alichokinunua baada ya kudunduliza fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kama njia ya kujiongezea kipato.
Mmoja wa Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Mabalasana katika halmashauri ya wilaya ya Geita akiwa mbele ya nyumba na matofari aliyopata kwa kutumia fedha za Mpango wa kunusuru Kaya Maskini katika jitihada za kuboresha makazi yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Geita.Ali Kidwaka akizungumza na Wandishi wa Habari juu ya utekelezaji wa Shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF hususani Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri yake ambapo amesema Mpango huo umekuwa chachu ya kaya za Walengwa kupiga vita umaskini kwa mafanikio makubwa na kutoa wito wa kutekeleza Mpango huo katika vijiji vyote.
Mmoja wa Walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF ,BI. Sabina Mtangwa (aliyevaa gauni jekundu ) mkazi wa kijiji cha Isamilo katika halmashauri ya wilaya ya Geita ,akimwonyesha Afisa Mawasiliano wa TASAF Estom Sanga mbuzi na ng’ombe waliozaliana baada ya kununua mbuzi na kuwauza aliowapata kwa kutumia fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »