BRIGEDIA JENERELI MSTAAFU AONGOZA MAZISHI YA KABURU KIGOMA

March 10, 2018

Na Rhoda Ezekiel, Kigoma

MKUU wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga amewaongoza mamia ya wakazi wa viongozi wa Serikali na vyama vya siasa katika mazishi ya aliyekuwa mwanasiasa mkongwe nchini na Mwenyekiti msaafu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani Kigoma, Amani Kaburu.

Akizungumza katika msiba huo Brigedia Jenerali Maganga amesema Kaburu ni mwanasiasa aliyejikita kutetea haki za wananchi wa Kigoma na alikuwa wa kwanza kupigania maendeleo ya mkoa huo.Mwili wa Kaburu umepumzishwa jana kwenye nyumba yake ya milele.

Amesema Serikali na CCM itamkumbuka Kaburu kwa mchango mkubwa ambao ameufanya katika mkoa huo na amekuwa mfano wa kuigwa na wengine na licha kutangulia mbele ya haki ameacha alama.

"Marehemu Kaburu atakumbukwa kwa mchango wake na alipokuwa kiongozi wa vyama mbalimbali na hata katika Bunge la Afrika Mashariki.Hakika ameondoka lakini wana Kigoma tutamkumbuka daima na kwa wanasiasa wengi wanafahamu kuwa vijana wengi mkoani hapa wamejifunza siasa kutoka kwake,"amesema na kuongeza kifo cha Kaburu kimeacha pigo kubwa kwa Serikali, CCM, wananchi wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma Amandusi Nzamba amesema CCM imepata pigo kubwa kwa kumpoteza mwanasiasa huyo aliyekuwa mstari wa mbele kukisaidia chama hicho katika kufikia malengo yao.Wakati huohuo Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Zitto Kabwe amesema kama mtoto na mwanafunzi wa Kaburu pamoja na tofauti za kisiasa ndiye aliyekuwa mwalimu wao na aliwazibua masikio wanasiasa wengi wa Mkoa huo.

"Kaburu enzi za uhai wake ametufundisha wengi na hasa kuhusu siasa za Tanzania na kubwa zaidi alihimiza umoja na mshikamano mbele ya maendeleo ya Kigoma.Huyu ni kiongozi wa kwanza kupitia mfumo wa vyama vingi na ndio mwalimu wetu katika siasa za vyama vingi.Alijitoa na kupambana na kupigania siasa za Mkoa wetu wa Kigoma na amefanya kazi kubwa,"amesema Zitto.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania(Bakwata) Mkoa wa Kigoma Salim Kangeta amesema Kaburu ni kiongozi aliyeshirikiana na kila mtu na hata viongozi wa dini na kubwa zaidi alikuwa anasikiliza ushauri kwa lengo la mkoa huo kusonga mbele kimaendeleo.


HISTORIA YA KABURU

Kaburu alizaliwa mwaka 1949 mkoani Kigoma na alisoma elimu yake ya msingi Shule ya Msingi Kipampa na elimu ya sekondari katika Shule ya Living Stone Kigoma.

Baada ya hapo aliondoka na kwenda kuendelea na masomo yake nchini Marekani ambapo baada ya hapo alirejea nchini na kuanza harakati za siasa. Alikuwa mbunge wa Jimbo la Kigoma kwa kipindi cha miaka tisa, pia amewahi kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki , Katibu Mkuu wa Chadema na amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma.

Katika msiba huo CCM imetoa Sh.900,000 kwa ajili ya rambirambi na CCM Makao Mkuu imetoa Sh.milioni moja wakati Serikali ya Mkoa wa Kigoma nayo imetoa Sh.milioni moja kwa niaba ya Serikali Kuu.Chama cha ACT-Wazalendo kimeshiriki kusafirisha mwili.
 
 Baadhi ya Ndugu,Jamaa na Marafiki wakiwa kwenye mazishi ya Dkt Kaborou hapo jana.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »