Wananchi wa Jimbo Busanda, wilayani Geita wametakiwa kujikumbusha hatua za maendeleo zilizofikiwa katika eneo lao na kujotokeza kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu.
Wito huo umetolewa Oktoba 24, 2025 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa na mgombea wa Ubunge Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Mashaka Biteko wakati akihutubia katika Mkutano wa Kufunga Kampeni Jimbo la Busanda.
“Nawaomba mjikumbushe kuhusu maendeleo yaliyofikiwa katika kipindimcha miaka michache iliyopita. Maendeleo yaliyofikiwa katika sekta ya elimu, sekta ya Afya, miundombinu ya Barabara na maendeleo katika sekta ya umeme makubwa” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza kuwa wana Busanda watakuwa na haki ya kudai maendeleo zaidi endapo watatimiza haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kupiga kura ifikapo Oktoba 29, mwaka huu.
Aidha amewaomba wananchi kumchagua mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mbunge na madiwani kutoka CCM ili waendeleze mafanikio yaliyopatikana.
Naye Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila amewataka wananchi kujiandaa na kujipanga kwa ajili ya tukio la upigaji kura ifikapo Oktoba 29, mwaka huu.
“ Jiandae na kujipanga kwa ajili ya kuwachagua viongozi waleta maendeleo ili kufanikisha hilo kila mwana CCM aliyejiandikisha ajitokeze kupiga kura” amesema Kasendamila.
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Busanda, Dkt. Jafari Seif amewashukuru wajumbe wa chama hicho kwa kumchagua kuwa mgombea wa kiti cha ubunge ili aweze kuwawakilisha.
Pia amemshukuru Dkt. Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.
Dkt. Seif pia amewaomba wana Busanda kumchagua Dkt. Samia, Mbunge na madiwani wa CCM ili waendeleze ushirikiano katika kutekeleza miradi ya maendeleo.






EmoticonEmoticon