Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Mhe. Luhaga 
Joelson Mpina(Mb) mwenye miwani akimkabidhi uenyekiti  wa Baraza  
la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye Maji katika 
nchi za Afrika Mashariki(FASCoM)  Mhe. Ssempija Vicente Bamulangaki 
ambaye ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Uganda hivi karibuni.
 Baraza  la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na Utunzaji 
wa Viumbe Kwenye Maji katika nchi za Afrika Mashariki(FASCoM) linaliwajumuisha  
Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi wa Tanzania, Uganda na Kenya, Makatibu Wakuu 
na Wakurugenzi katika picha ya pamoja  baada ya kikao cha kwanza 
cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni Entebbe nchini Uganda.
Picha ya pamoja ya ujumbe wa Tanzania ulioongozwa 
na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina(mwenye 
miwani) baada ya kikao cha kwanza cha Baraza  la Mawaziri wa Sekta 
ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye Maji katika nchi za Afrika Mashariki(FASCoM) 
kilichofanyika hivi karibuni Entebbe nchini Uganda.Kushoto kwake ni 
Katibu Mkuu wa Uvuvi, Dkt Yohana Budeba.
 Na Mwandishi Maalum, Entebbe 
Zatenga  bilioni 4 za kufanya 
doria ya pamoja kunusuru kutoweka kwa Sangara. 
NCHI za Tanzania, Kenya na Uganda kwa pamoja zimeridhia 
kufanya operesheni ya pamoja ya kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa 
Victoria ili kuokoa samaki aina ya sangara walioko katika hatari kubwa 
ya kutoweka .
Uamuzi huo umefikiwa na Baraza la Mawaziri wa Sekta 
ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria  ( LVFO) ambapo wameidhinisha Dola za 
Kimarekani 1,800,000 sawa na sh. Bilioni 4.1  za kitanzania kwa ajili 
ya kufanya operesheni hiyo katika Ziwa Victoria.
Hivyo nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kila moja 
itapata Dola za Kimarekani 600,000 sawa na Sh. Bilioni 1.3 ili kufanikisha 
operesheni hiyo ya kuokoa samaki aina ya sangara walioko katika tishio 
la kutoweka katika Ziwa Victoria kutokana na kushamiri uvuvi haramu.
Kwa siku za karibuni kulikuwa na malalamiko kuwa 
operesheni hiyo inafanyika upande mmoja tu wa ziwa hilo kwa Tanzania 
huku shughuli za uvuvi haramu zikidaiwa kufanyika katika nchi za Kenya 
na Uganda hivyo uamuzi huo utasaidia kumaliza tatizo hilo lilidumu kwa 
miaka mingi sasa.
Akizungumza katika kikao kukabidhi madaraka kwa nchi 
ya Uganda mjini Entebbe juzi, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Baraza 
hilo ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Luhaga Mpina 
alisema fedha hizo zitasaidia kuongeza kasi ya kupambana na uvuvi haramu 
ambapo kwa Tanzania ilishaanza operesheni hiyo mwanzoni mwa mwaka huu 
na kuleta mafanikio makubwa.
Mpina pia aliwaomba viongozi wa nchi wanachama wanaozunguka 
Ziwa Victoria kutekeleza kwa vitendo mapendekezo yaliyotolewa na Taasisi 
za Utafiti za  KMFRI, TAFIRI na NaFIRRI ikiwemo kanuni ya urefu wa samaki 
aina ya sangara wanaoruhusiwa kuvuliwa (slot size regulations) kati 
ya sentimita 50 hadi 85, Kanuni hii licha ya kuagizwa na Kikao cha Baraza 
la Mawaziri 2016  kutumika kwa nchi zote lakini baadhi ya nchi hazijatekeleza 
sharti hili kikamilifu.
Aidha Waziri Mpina pia  aliwakumbusha viongozi wa 
nchi zinazotumia Ziwa Victoria kuwaeleza ukweli wananchi wao wanaojishughulisha 
na biashara ya uvuvi kuhusu Sheria za Uvuvi za nchi zingine ili kujiepusha 
na adha watakazokumbana nazo pindi nchi husika inapochukua hatua  kwa 
mujibu wa sheria zake na kwamba  Tanzania itaendelea kuheshimu sheria 
za nchi nyingine ili kulinda rasimali za ziwa hilo.
“Ni imani yangu kuwa itakuwa hivyo hivyo Kenya 
na  itakuwa hivyo hivyo Uganda kwani rasilimali hii ni mali yetu sote 
hivyo tunajukumu kubwa la kuilinda kwa manufaa ya kizazi cha sasa na 
kijacho”alisema.
Hivyo Waziri Mpina alisisitiza kuwa biashara ya uvuvi 
haramu itabaki historia katika nchi za Afrika Mashariki kama viongozi 
watakuwa na dhamira safi na kujitoa kwa moyo wote kulinda rasilimali 
hizo na kwamba vita hiyo haiwezi kufanikiwa kama viongozi hawatajitoa 
mhanga kufanikisha kazi hiyo.
Hata hivyo chini ya uenyekiti wake, Waziri Mpina 
alijivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana ikiwemo kuanzishwa vya vikosi 
kazi mtambuka vilivyoweza kongoza mapambano ya uvuvi haramu ikiwemo 
Inter-Agency Unit ya Kenya, Multi-Agency Task Team(MATT) ya Tanzania 
na Fisheries Protection Force(FPF) ya Uganda.
Alisema  Tanzania imepata mafanikio makubwa baada 
ya kuendeshwa kwa operesheni Sangara 2018 ambayo ililenga kupambana 
na uvuvi haramu kwa kuondoa zana zote haramu ndani ya ziwa, kudhibiti 
wazalishaji zana haramu pamoja na wachakataji wa samaki wasioruhusiwa.
Aidha Waziri Mpina alimweleza Mwenyekiti mpya wa 
Baraza hilo ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Uganda, 
Ssempijja Vicent Bamulaki kutambua kuwa kupewa fursa ya kuongoza watu 
ni kupewa  fursa ya kuleta  mageuzi na kwamba uongozi ni vitendo sio nafasi.
Waziri Mpina alieleza kuwa hali ya upatikanaji wa 
samaki aina ya sangara ni mbaya katika Ziwa Victoria kwani kwa mujibu 
wa taarifa kutoka Taasisi za Utafiti za Afrika Mashariki zinaonyesha 
kuwa sangara wenye urefu wa sentimita 50 na kuendelea wamepungua na 
kubakia asilimia 5 tu, hivyo juhudi za haraka zisipochukuliwa samaki 
hao watatoweka na shughuli za uvuvi katika ziwa hilo zitakoma .
Aidha, Waziri alisema  katika kipindi cha uongozi 
wake kumekuwepo na changamoto mbalimbali zikiwemo uvuvi haramu,utoroshaji 
wa mazao ya uvuvi,usimamizi dhaifu wa sheria, uvunaji holela,nguvu kubwa 
ya uvuvi,ukwepaji wa mapato ya Serikali, nchi wanachama na nchi za nje 
kuingia katika mipaka ya nchi nyingine na kufanya biashara ya uvuvi 
bila vibali wala leseni.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa LVFO anayemaliza 
muda wake, Godfrey Monor alisema nafasi ya Katibu Mtendaji kwa kipindi 
hiki ni ya Tanzania na nafasi na Katibu Mtendaji Msaidizi ni ya nchi 
ya Uganda baada ya Sekretarieti iliyopo kumaliza muda wake Agosti mwaka 
huu kwa mujibu wa mkataba wa LVFO kifungu cha X hivyo nchi husika zifanye 
mchakato wa kujaza nafasi hizo kwa muda muafaka.
Monor alisema miongoni mwa maazimio ya kikao hicho 
ni pamoja na kuundwa kwa chombo kipya kitakachosimamia rasilimali za 
uvuvi katika nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (East 
Africa Fisheries Organizatin – EAFO) ili kusimamia shughuli zote za 
uvuvi katika mito,maziwa na bahari badala ilivyokuwa awali kwa LVFO 
kusimamia Ziwa Victoria pekee.
Waziri Mpina alisema  miongoni  mwa ajenda 
za  kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi Kanda 
ya Ziwa Victoria ( LVFO) ilikuwa ni kujadili utekelezaji wa  maagizo 
ya  kikao cha awali cha tisa cha Baraza hilo kilichofanyika Nairobi 
nchini Kenya Januari 29 mwaka 2016. 
Baadhi maagizo yaliyowasilishwa ni pamoja  na 
kuwasilisha taarifa za tafiti za kisayansi kutoka katika taasisi zenye 
dhamana ya kufanya tafiti za uvuvi kwenye nchi wanachama ili kusaidia 
usimamizi wa pamoja wa  Ziwa Victoria ambapo  taasisi hizo kwa 
upande wa Tanzania ni TAFIRI, Kenya ni KMFRI na  NaFIRRI kwa upande 
wa Uganda.
Mheshimiwa Mpina alisema kikao hiki kimekuwa ni kikao 
cha kwanza baada ya mabadiliko  makubwa yaliyofanywa katika kikao 
cha tisa cha Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria  
( LVFO) kilichofanyika Nairobi nchini Kenya Januari 29 mwaka 2016 ambacho 
kilifanya mabadiliko ambayo yanalifanya baraza hilo kuwa Baraza  
la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye Maji katika nchi za Afrika Mashariki(FASCoM)  badala 
ya (LVFO)


