SHUWASA,POLISI WATEKETEZA VIFAA VINAVYOTUMIKA KUHARIBU VYANZO VYA MAJI BWAWA LA NING'WA SHINYANGA

December 20, 2017
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA) kwa kushirikiana na jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga wameendesha zoezi la kuteketeza vifaa vinavyotumika kuharibu vyanzo vya maji katika bwawa la Ning’wa.

Miongoni mwa vifaa vilivyoteketezwa kwa moto ni nyavu za kuvulia samaki,mitumbwi na vibanda vinavyotumiwa na wavuvi kujihifadhi karibu na bwawa hilo.Zoezi hilo limefanyika leo Jumanne Desemba 19,2017 katika bwawa hilo lenye mita za ujazo milioni 10.9 linalopatikana katika kata za Old Shinyanga,Chibe na Pandagichiza zilizopo katika wilaya ya Shinyanga. 

Akizungumza wakati wa zoezi hilo,Mkurugenzi wa SHUWASA,Injinia Sylivester Mahole alisema lengo la oparesheni hiyo aliyodai ni endelevu, ni kuhifadhi vyanzo vya maji kwani bwawa hilo ni moja vya vyanzo muhimu vya maji vya mamlaka hiyo ukiachilia mbali Ziwa Victoria. 

“Tumeteketeza kwa moto vifaa vilivyokuwa vinatumika kwa shughuli za uvuvi katika bwawa hili ikiwemo mitumbwi,nyavu na vibanda vilivyokuwa vinatumiwa na wavuvi,tunataka waache mara moja kufanya uvuvi hapa kwani wanaharibu vyanzo vya maji”,alieleza Injinia Mahole. 

Aidha alisema shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo,uvuvi na ufugaji zinaharibu vyanzo vya maji katika bwawa hilo ambapo kina chake kimekuwa kikipungua mara kwa mara. 

“Umeibuka utamaduni wa wananchi kulima bustani pembezoni mwa bwawa kisha kuweka pampu majini wakati huo watumia dawa za mazao ambazo siyo nzuri kwa afya ya binadamu,wananywesha mifugo hapa na kuvua samaki kwa kutumia nyavu na vyandarua”,alifafanua Injinia Mahole. 

Alisema pamoja na kuendelea kufanya vikao na mikutano na wananchi kuwapa elimu ya hifadhi ya vyanzo vya maji bado wananchi wamekuwa wakifanya shughuli za kibinadamu katika bwawa hilo hivyo wataendelea oparesheni ya kuharibu vifaa na kukamata watu wote wanaokiuka sheria na kanuni za utunzaji mazingira na vyanzo vya maji. "Tulifanya vikao na mikutano na viongozi pamoja na wananchi wao ndiyo wakatoa azimio la kuondoa watu wote wanaofanya shughuli za kibinadamu katika bwawa hili huku wakiipa SHUWASA jukumu la kusimamia zoezi zima,na sisi tangu mwezi Septemba mwaka huu tumekuwa tukiendesha oparesheni ya kuondoa watu wanaoharibu vyanzo vya maji",aliongeza. 

Aidha aliwataka wananchi kuzingatia kanuni na sheria za hifadhi ya vyanzo vya maji na kwamba hawatasita kuwachukulia hatua wale watakaobainika kuendelea kuharibu vyanzo vya maji katika bwawa hilo. Vyanzo vikuu vya maji vya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA) ni Ziwa Victoria na bwawa la Ning’wa. 

Mpaka mwezi Novemba 2017 idadi ya maunganisho ya maji yaliyofanywa na SHUWASA mjini Shinyanga ni 18,900 ambapo zaidi ya watu 200,000 wanapata huduma ya maji kutoka SHUWASA. 
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA),Injinia Sylivester Mahole akielezea lengo la kuendesha oparesheni ya kuteketeza kwa moto vifaa vinavyotumiwa na wananchi kuharibu vyanzo vya maji katika bwawa la Ning'wa.Kulia ni mwandishi wa habari wa Radio Faraja na DW,Veronica Natalis - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog 
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA),Injinia Sylivester Mahole akionesha mifugo katika bwawa la Ning'wa 
Kushoto ni ng'ombe wakiingia katika bwawa la Ning'wa, katikati ni askari polisi akitoa maelekezo kwa wananchi waliokutwa katika bwawa hilo na kuambiwa waondoe mitego ya samaki iliyowekwa katika bwawa hilo. 
Askari polisi akishirikiana na mwananchi kuondoa mtego wa samaki katika bwawa la Ning'wa 
Zoezi la kuondoa mtego wa samaki likiendelea 
Askari polisi aliyevaa kiraia akiondoa nyavu ya chandarua katika bwawa la Ning'wa 
Zoezi la kubomoa mtumbwi likiendelea
Askari polisi wakiendelea kubomoa mtumbwi kwa kutumia nyundo 
Askari polisi akimwaga mafuta kwa ajili ya kuchoma moto nyavu zinazotumika kuvua samaki katika bwawa la Ning'wa 
Moto ukiteketeza nyavu 
Nyavu zikiteketea kwa moto 
Zoezi la kuchoma moto nyavu likiendelea 
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA),Injinia Sylivester Mahole akizungumza na mmoja wa wananchi aliyekutwa akifanya shughuli za kibinadamu katika bwawa hilo Jackson Kabanda 
Askari polisi wakiangalia vibanda vinavyotumiwa na wavuvi kujihifadhi karibu na bwawa la Ning'wa. 
Vibanda vinavyotumiwa na wavuvi katika bwawa la Ning'wa vikiteketezwa kwa moto 
Moto ukiteketeza vibanda vya wavuvi katika bwawa la Ning'wa. 

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »