Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na
Umwagiliaji Mhe.Juma Aweso akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali za wabunge
wakati wa kikao cha pili cha Mkutano wa tisa wa Bunge leo Mjini Dodoma.
………………….
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Serikali imewaagiza wakurugenzi wa
Halmashauri kuwachukulia hatua wakandarasi wa maji wanaokiuka mikataba
walioingia kwa kuchelewa kutekeleza miradi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni
mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mufindi Kusini Mendrad Lutengano
Kigola juu ya lini Serikali itamaliza kujenga mradi wa Kata ya Mtwango
katika Vijiji vya Sawala, Mtwango, Rufana na Kibao.
“Viijiji vya Sawala, Mtwango,
Rufana na Kibao katika kata ya Mtwango ni miongoni mwa vijiji 12
vilivyopendekezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kupatiwa huduma ya
maji kupitia programu ndogo ya maji na usafi wa mazingira vijijjini,”
alisema Awezo.
Aliendelea kwa kusema, utekelezaji
wa mradi huo ulianza Juni 01, 2015 na ulitakiwa kukamilika Juni 01,
2016 kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.36 ambapo awamu ya kwanza ilikuwa
ni ujenzi wa miundombinu ya maji katika kijiji cha Sawala pekee ambapo
hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 50.
“Hadi mwezi Novemba, 2016
mkandarasi alikuwa hajakamilisha kazi na hivyo Halmashauri kuamua
kuvunja mkataba na halmashauri ilitangaza upya zabuni kwa ajili ya
ukamilishaji wa kazi zilizobaki,” alifafanua Aweso.
Amesema kuwa, mkandarasi mwingine
amepatikana na utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza Desemba, 2017
kwa muda wa miezi 12 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.81.
Kutokana na ucheleweshaji wa mradi
huo, Aweso amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini
kuwachukulia hatua wakandarasi wa maji ambao hawatekelezi miradi yao kwa
muda uliopangwa ambao kwa kiasi kikubwa unawaathiri wananchi
wanaohitaji huduma ya maji kutokana na mradi kutekelezwa kwa muda mrefu.
EmoticonEmoticon