Na Mwandishi wa diGOtv, Tanga
WATU wenye ulemavu mkoani Tanga wamepata tabasamu jipya kufuatia Ofisi ya Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga, Mhandisi Mwanaisha Ulenge, kutangaza neema ya kugawa miguu bandia 100, viti mwendo (wheelchairs), na fimbo kwa wasioona, sambamba na kuwafungulia fursa za kiuchumi kupitia mafunzo maalum.
Hatua hii ni mwendelezo wa mikakati thabiti ya Mbunge huyo katika kuwajali, kuwainua kiuchumi, na kurudisha matumaini kwa wananchi wenye mahitaji maalum mkoani hapa ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa na kujikwamua kimaisha.
Ugawaji wa Viti Mwendo na Fimbo (Kesho Ijumaa)
Katika kuhakikisha makundi yote yanafikiwa, Mhe. Ulenge kesho *Ijumaa (Julai 10, 2026)* anatarajia kugawa vifaa saidizi vifuatavyo kwa walengwa:
* *Viti Mwendo (Wheelchairs):* 20
* *Fimbo za watu wenye uoni hafifu:* 25
*MUHIMU KWA WENYE UHITAJI:* Watu wote wenye uhitaji wa viti mwendo na fimbo hizo wanaombwa kuwasiliana haraka kupitia namba ya simu *0753 210 211* ili kupewa maelekezo ya namna ya kuvipata.
*Zoezi la Kujaribisha Miguu Bandia (Limeanza Leo)*
Akitoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu miguu bandia 100, Mhe. Ulenge amebainisha kuwa zoezi la kitabibu la kujaribisha miguu hiyo (*fittings*) kwa walengwa ambao tayari walishapimwa hatua ya awali na wataalamu kutoka *Taasisi ya Kamal Foundation*, *limeanza rasmi leo Alhamisi, Julai 9, 2026.*
Zoezi hili litaendelea hadi *Jumatatu, Julai 13, 2026*, kuanzia saa 2:00 asubuhi kila siku katika ukumbi wa *Regal Naivera* uliopo Tanga Mjini. Walengwa wote wanasisitizwa kufika bila kukosa.
*Matembezi ya Hisani na Hafla Kuu ya Makabidhiano*
Baada ya kukamilika kwa hatua ya kujaribisha viungo hivyo, kilele cha tukio hilo la kihistoria linatarajiwa kuwa *Jumanne ya Julai 14, 2026*.
Siku hii muhimu itatanguliwa na *matembezi makubwa ya hisani* yatakayozunguka mitaa mbalimbali ya Jiji la Tanga kuhamasisha jamii, na kisha kuhitimishwa katika ukumbi wa Regal Naivera. Hapo ukumbini ndipo hafla kubwa ya kukabidhi miguu hiyo bandia kwa walemavu wote 100 itakapofanyika rasmi. Hatua hiyo inatarajiwa kuwasaidia walengwa wengi kurudisha uwezo wao wa kutembea na kufanya shughuli zao za uzalishaji mali kwa urahisi tofauti na ilivyokuwa awali.
*Mafunzo ya Sheria ya Asilimia 30 (Fursa za Kiuchumi)*
Ili kuhakikisha kundi hilo linapata ukombozi kamili wa kiuchumi badala ya kutegemea misaada pekee, hafla hiyo itaambatana na utoaji wa mafunzo maalum ya uwezeshaji.
Mhe. Ulenge alisema washiriki watapatiwa elimu ya kina kuhusu namna ya kunufaika na fursa za kisheria zinazoelekeza Mamlaka za Serikali kutenga asilimia 30 ya zabuni kwenye manunuzi ya umma kwa ajili ya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu. Mafunzo haya yanalenga kuwapa ujasiri wa kuomba zabuni na kufanya biashara rasmi na taasisi za Serikali.
.jpg)
EmoticonEmoticon