Benny Mwaipaja, Dar es
Salaam
KATIBU Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. Doto James amewatoa hofu watanzania kuhusu ongezeko la
Deni la Taifa akisisitiza kuwa Deni hilo ni himilivu.
Bw. James amesema hayo
Jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari wakati wa hafla fupi ya kutia saini
Mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa Shilingi bilioni 340 uliotolewa na
Benki ya Dunia kwa ajili ya Mradi wa kuendeleza utalii kwa vivutio vilivyoko
katika ukanda wa kusini mwa Tanzania ujulikao kama Resilient Natural Resource
for Tourism and Growth (REGROW)
Alikuwa akitolea ufafanuzi
kuhusu baadhi ya watu na vyombo vya habari vinavyozungumzia Deni la Taifa kwa
kutumia neno Deni la Taifa “linapaa”
Katibu Mkuu huyo ambaye
pia ndiye Mlipaji Mkuu wa Serikali alisema kuwa Deni la Taifa ni himilivu kwa
kutumia viwango vya kitaifa na kimataifa kwamba ili nchi iwe katika hatari ya
kukua kwa Deni lake la Taifa inabidi lifikie asilimia zaidi ya 50 lakini kwa
Tanzania kiwango cha deni hilo ni asilimia 32.
“Deni letu lingekuwa
linapaa, hata Benki ya Dunia wasingekubali kutukopesha kwa maana hiyo tukitaka
kukopa tutafanya hivyo kwa kuwa tuko chini katika viwango vya ukopaji kwa
asilimia zaidi ya 18” alisema Bw. Doto James.
Kwa hiyo nawaomba hili
mlichukue muuelimishe umma wa watanzania kwamba deni la Taifa ni stahimilivu,
nchi inakopesheka vizuri.
Novemba 7, 2017, Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwasilisha Bungeni mjini Dodoma
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maanndalizi ya
Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/2019 alisema kuwa Deni la Taifa limefikia dola
za Marekani milioni 26,115.2 mwezi Juni mwaka 2017.
Dkt. Mpango alieleza kuwa ongezeko hilo ni
sawa na asilimia 17 ikilinganishwa na dola milioni 22,320.76 katika kipindi
kama hicho mwaka 2016.
Alisema ongezeko hilo lilichangiwa na mikopo mipya
iliyochukuliwa ili kugharamia miradi ya maendeleo kama vile: Standard Gauge Railway; Strategic Cities; mradi wa usafirishaji Dar es Salaam
(DART) na kupanua upatikanaji wa maji safi Dar es Salaam.
Deni hilo la Taifa linajumuisha deni la Serikali
lililofikia dola za Marekani milioni 22,443.70 na deni la sekta binafsi la dola
za Marekani milioni 3,671.50. Pamoja na ongezeko hili, viashiria vyote bado
vinaonesha kuwa deni la Taifa ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati
na mrefu huku uwiano kati ya deni na Pato la Taifa umefikia asilimia 31.2
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56.
EmoticonEmoticon