Wataalamu
waanza kuwanoa wanafunzi, walimu na maafisa elimu kukabiliana na matokeo duni
ya mitihani
Na Oscar Assenga, Tanga
MATOKEO duni ya mitihani ya Taifa
katika baadhi ya shule za sekondari za Serikali jijini Tanga yameibua hatua
mpya za kuwanufaisha wanafunzi kupitia mafunzo maalumu yanayolenga kuongeza
ufaulu kwa kuwajengea uwezo wa kujifunza kwa ufanisi na kujiandaa vizuri kwa
mitihani.
Mafunzo hayo yanatekelezwa na
Taasisi ya Tanzania Centre for Education (TCE) kwa kushirikiana na Taasisi ya
Botnar foundation na Inovex kupitia mradi wa Tanga Yetu, unaohusisha
shule 10 zilizobainika kuwa na changamoto ya matokeo hafifu kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa kuanza kwa
mafunzo hayo katika Shule ya Sekondari Nguvumali, Mkurugenzi Mtendaji wa TCE, Yusuf
Ogutu, alisema kuboresha ufaulu ni hatua muhimu ya kuinua ubora wa elimu na
kuwawezesha wanafunzi kufikia ndoto zao za kitaaluma na maisha ya baadae.
Alisema wanafunzi wengi hufanya
mitihani bila kuelewa kwa kina mfumo wa maswali ya umahiri, uzito wa mada na
mbinu sahihi za kujibu, hali inayochangia kushuka kwa matokeo licha ya
kufundishwa darasani.
"Ndiyo maana tumeamua kuja na mafunzo
haya ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa kuelewa, badala ya kukariri.
Tunawafundisha namna ya kuchambua muhtasari wa masomo, kutambua mada
zinazotiliwa mkazo katika mitihani na kuelewa matumizi ya vitenzi vinavyotumika
katika maswali," alisema.
Aliongeza kuwa wanafunzi pia
wanapatiwa mbinu za kupanga muda wa kujisomea, namna ya kujiandaa kabla,wakati
na baada ya mtihani, jinsi ya kujibu maswali kwa ufanisi na namna ya
kujitathmini baada ya kufanya mtihani.
Ogutu alisema mafanikio ya wanafunzi
hayawezi kupatikana kwa juhudi za mwanafunzi pekee, bali yanahitaji ushirikiano
wa walimu, wazazi, viongozi wa elimu na wadau wa maendeleo.
"Tunataka kujenga utamaduni wa
ufaulu. Mwanafunzi akielewa namna ya kujifunza na mwalimu akapata mbinu bora za
kumwelekeza, matokeo mazuri yatapatikana," alisema.
Mbali na mafunzo hayo, alisema
taasisi hiyo imeanza kufanya utafiti katika shule zote 27 za sekondari za
Serikali za Jiji la Tanga ili kubaini sababu zinazochangia kushuka kwa ufaulu
katika mitihani ya Kidato cha Pili na Kidato cha Nne.
Alisema matokeo ya utafiti huo
yatawezesha wadau wa elimu kuweka mikakati ya muda mrefu ya kuboresha ubora wa
elimu na kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule za Serikali.
Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu
Kata ya Nguvumali, Lilian Shetua, alisema mafunzo hayo yanawasaidia
wanafunzi kuendana na mahitaji ya mtaala ulioboreshwa unaowataka kuwa wabunifu,
wachambuzi na wenye uwezo wa kutumia maarifa katika kutatua changamoto.
Alisema wanafunzi wengi wamekuwa
wakifanya mitihani bila kuelewa muundo wake, lakini kupitia mafunzo hayo
wanapata uelewa wa namna ya kujiandaa na kujibu maswali kwa kuzingatia matakwa
ya Baraza la Mitihani.
"Ni matarajio yetu kwamba elimu
hii itabadilisha mtazamo wa wanafunzi na kuongeza kiwango cha ufaulu katika
shule yetu na nyingine zinazoshiriki mradi huu," alisema.
Naye Inspekta wa Polisi wa Kata ya
Nguvumali, Sharifu Kiswamba, alisema pamoja na jitihada za kuboresha
elimu, bado utoro wa wanafunzi na tabia ya kuzurura mitaani wakati wa masomo
vinaendelea kuwa kikwazo kikubwa.
Aliwataka wazazi kuongeza usimamizi
wa watoto wao na kushirikiana na walimu pamoja na viongozi wa kata ili
kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo na kutumia muda wao kujifunza.
Kwa upande wake, mwalimu wa Shule ya
Sekondari Nguvumali, Venosa Massawe, alisema mafunzo hayo yamekuja
wakati mwafaka kwani yanawasaidia walimu na wanafunzi kutafsiri kwa usahihi
matakwa ya mtaala ulioboreshwa.
Hata hivyo, alisema mazingira magumu
ya maisha ya baadhi ya wanafunzi, ikiwamo umaskini, malezi yasiyo ya karibu na
changamoto za lishe, bado ni miongoni mwa sababu zinazochangia kushuka kwa
kiwango cha ufaulu.
Alisema ushirikiano wa Serikali,
wazazi, walimu na wadau wa maendeleo utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga
mazingira bora ya kujifunza na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofaulu kwa
viwango vya juu katika mitihani ya taifa.











EmoticonEmoticon